Habari

Familia yaishi na duma iliyemuokoa kutoka msituni

Na KITAVI MUTUA October 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MNAMO Aprili 2023, Bi Bishara Abdinoor aliingiwa na hofu alipomwona mwanae wa kiume amerejea nyumbani akimbeba mtoto wa duma.

Tineja huyo alikuwa ameshinda mchana kutwa akilisha ng’ombe katika kijiji chao cha Kursi kinachopakana na Hifadhi ya Wanyamapori ya Sabuli, alipompata mnyama huyo mdogo akiwa ametelekezwa na mamake.

Mama Abdinoor hakuwa na ufahamu kuwa ni hatia kuwa na mnyama wa porini bila leseni kutoka kwa Shirika la Wanyamapori Nchini (KWS) na hatari ambayo mwanawe aliwaletea kwa kumleta nyumbani mtoto wa duma.

“Nilitaka kumtupa mtoto huyo wa duma kwa hofu kwamba mamake angefuatilia harufu yake na aje kumchukua. Lakini mwanangu aliniomba nimruhusu amlishe kabla ya kumruhusu arejee mwituni,” akaelezea kwenye mawasiliano ya simu na Taifa Leo Dijitali.

Mahojiano hayo yalikuwa yamepangwa na Naibu Mkurugenzi anayesimamia eneo la Uhifadhi la Kaskazini Bakari Chongwa, ambapo Bi Abdinoor aliongea kupitia mkalimani.

“Mwanangu alimlisha mtoto huyo wa duma kwa chakula ambacho tuliandaa jioni hiyo; mchele kwa kitoweo cha nyama. Aidha, alimtengenezea kizimba cha kulala,” akaeleza.

Lakini familia ya Bi Abdinoor iliogopa kuwa duma huyo akiwa mkubwa angeanza kula mifugo wao, haswa mbuzi, kando na kuwashambulia watu.

Na hata baada ya kumrejesha msituni, alirejea nyumbani kwa Bi Abdinoort kila wakati, kwani alionekana kupenda chakula kilichopikwa.

“Baada ya miezi kadhaa tuliingiliana na mnyama huyo wa mwituni, alipenda watu na angetambua kila mtu katika familia yetu. Sasa tulianza kumfunga chini ya kivuli cha mti huku tukimlisha kwa hofu kwamba angewashambulia watu,” akasema.

Siku moja Afisa wa KWS anayesimamia Kaunti ya Wajir Rashid Jumale alialikwa katika redio moja inayopeperusha matangazo kwa lugha yamama, ambapo alihimiza wanajamii kuripoti visa vya wanyamapori kuingia katika makazi ya watu na hapo ndio familia iliwasiliana na KWS.

Baada ya kusikiza ushauri huo, Bw Abdinoor alituma ujumbe kwa KWS kwamba wanafuga duma ambaye walimwokoa kutoka msitu.

Bw Chongwa alimshukuru mwanamke huyo kwa kutumza mwana duma huyo sawa na mbwa au paka wake.Maafisa KWS walimchukua mnyama huyo na kumsafirisha hadi hifadhi ya Nairobi Safari Walk, ambako anatunzwa.