Familia yataka Kanja ashinikizwe aseme aliko meneja wa Huduma Centre aliyetoweka
FAMILIA ya meneja wa Kituo cha Huduma Centre katika Kaunti ya Wajir Hussein Abdirahman aliyetoweka siku sita zilizopita jana ilimshtaki Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Douglas Kanja ikiomba mahakama kuu imshurutishe amfikishe kortini aidha akiwa hai ama akiwa amekufa.
Kupitia kwa mawakili Danstan Omari na Shadrack Wambui, familia hiyo ilisema Abidirahman, aliye pia Naibu wa Kamishina alipotea siku moja baada ya kumlaki Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku kuzuru kaunti hiyo Julai 7, 2025.
Katika kesi iliyowasilishwa katika Mahakama Kuu ya Milimani, familia hiyo imeomba IG, Mwanasheria Mkuu na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) washurutishwe kumfikisha kortini Abdirahaman.
Tangu Julai 8, 2025 familia hiyo imesema kwamba imemtafuta bila mafanikio.
“Familia ya Abdirahman imesononeka sana kufuatia kutoweka kwake wala hakuwa na uhasama na mtu yeyote,” Bw Wambui alisema baada ya kuwasilisha kesi mahakamani.
Bw Wambui alisema haki za mtumishi huyo wa umma zimekandamizwa na polisi hawapaswi kusema hawajui aliko Abdirahman.
Mahakama kuu itatoa mwelekeo kumshurutisha IG amfikishe kortini mwathiriwa.
Mawakili hao walisema kumekuwa na mtindo wa polisi kuwateka nyara wananchi na hatimaye kuwaachilia ama kuwaua.
Kesi hiyo ilipelekwa kwa Jaji Lawrence Mugambi kwa maagizo.