Habari

Fedha za e-Citizen hazifiki Benki Kuu, Bunge laambiwa

Na DAVID MWERE July 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KAMATI ya Bunge la Kitaifa kuhusu Hesabu za Serikali (PAC) imeamuru Katibu wa Wizara ya Fedha, Dkt Chris Kiptoo ajiwasilishe  kwake kuhusiana na masuala ya e-Citizen huku ikiibuka hela za Wakenya zinazokusanywa kupitia tovuti hiyo huenda hazifiki akaunti za Hazina ya Kitaifa katika Benki Kuu ya Kenya (CBK).

PAC ilichukua hatua hiyo huku ikikosoa Hazina Kuu kwa kufeli kutekeleza mapendekezo ya kamati hiyo kuhusu kulainisha mfumo huo wa kulipia huduma za serikali kimtandao kuhakikisha utendakazi bora na uwajibikaji kuhusu fedha za umma.

Kwa kukosa kutekeleza mapendekezo hayo, Hazina Kuu imesababisha matatizo kwenye tovuti hiyo yanayozidi kujitokeza katika asasi mbalimbali jinsi yanavyoangaziwa na Mkaguzi Mkuu Nancy Gathungu.

Wakili Mkuu Shadrack Mose, alipofika mbele ya PAC kuhusu akaunti za Afisi ya Mwanasheria Mkuu katika bajeti ya 2022/23, alikabiliwa na wakati mgumu huku akishindwa kufichua kiasi kinachokusanywa na Afisi hiyo kupitia e-Citizen kutokana na huduma zinazotolewa kama vile vyeti vya ndoa.

Bw Mose alisema hakuwa na rekodi kutoka kwa Hazina Kuu kuhusu kiasi cha mapato yanayokusanywa na Afisi ya Mwanasheria Mkuu kupitia e-Citizen na iwapo yanahifadhiwa CBK.

“E-citizen haitupi ripoti kuhusu kiasi tunachokusanya,” alisema Bw Mose kabla ya mwenyekiti wa PAC, Tindi Mwale (Butere) kuagiza Bw Kiptoo kufika mbele ya kamati kufafanua suala hilo.

“Katibu wa Wizara ni sharti aje afafanue suala hili kwa sababu linaadhiri idara za serikali,” alisema Bw Mwale kufuatia maswali kutoka kwa wanakamati kuhusu Hazina Kuu kukosa kutekeleza mapendekezo ya PAC.

E-citizen iliyozinduliwa 2014, ni mpango wa Wizara ya Fedha unaosimamiwa na Mamlaka ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT) Nchini (IDA).

Katika ripoti yake kwa Bunge la Kitaifa kuhusu ukaguzi wa akaunti za wizara, idara na asasi za serikali (MDAs), PAC imetoa mapendekezo kadhaa kwa Hazina Kuu kuhusu tovuti ya e-Citizen na masuala yanayojitokeza kila mara kuhusu usimamizi wake.

Mbunge wa Turkana, Joseph Namwar alisema e-Citizen inatumiwa vibaya na walio mamlakani.