Chama cha Sufuria chaundwa, chaomba kusajiliwa
CHAMA kipya cha kisiasa kinachoitwa Kenya Great Party (KGP), ambacho alama yake ni sufuria, kimewasilisha maombi ya kusajiliwa rasmi — hatua ambayo imezua mjadala mkubwa miongoni mwa Wakenya wanaokumbuka maandamano ya kupinga serikali ya mwaka 2023 yaliyoongozwa na muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Alliance.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Bw John Cox Lorionokou, ofisi yake imepokea ombi la usajili wa muda wa chama hicho, ambacho waanzilishi wake ni Wakenya sita — Mercy Njeri Chomba, Sheila Jemutai, David Muiruri Njoroge, Ivan Matunda Bundi, Peter Ngui, na Nasra Osman Ibrahim.
Kulingana na tangazo hilo, alama ya chama ni sufuria, rangi zake ni kijivu, bluu nyepesi na nyeupe, na kaulimbiu yake ni “Kikazi Kipya.”
“Pingamizi lolote linaweza kuwasilishwa ndani ya siku saba tangu kuchapishwa kwa tangazo hili, kwa maandishi au ana kwa ana,” alisema Bw Lorionokou.
Ombi hilo limefufua kumbukumbu za maandamano ya mwaka 2023, ambapo wafuasi wa Azimio walitumia sufuria kama ishara ya njaa, gharama ya juu ya maisha na kukata tamaa kiuchumi. Wakati huo, viongozi wa upinzani wakiongozwa na Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, Martha Karua, Eugene Wamalwa na Jeremiah Kioni waliongoza maandamano jijini Nairobi wakiwa wamevaa sufuria vichwani.
Sufuria hizo ziligeuka kuwa alama kuu ya kisiasa ishara ya jikoni bila chakula, hasira ya wananchi, na upinzani dhidi ya utawala wa Rais William Ruto.
Miaka miwili baadaye, sufuria hiyo imejitokeza tena, si kama chombo cha maandamano, bali kama alama rasmi ya chama cha kisiasa kinachotaka kutambuliwa katika uwanja mpana wa siasa za vyama vingi nchini.
Wachambuzi wa siasa wanasema hatua hiyo inaonyesha jinsi utamaduni wa maandamano nchini Kenya mara nyingi unazalisha mawazo mapya ya kisiasa. Wanasema chama hicho kinaonekana kutaka kugeuza hasira na kilio cha wananchi wa kipato cha chini kuwa nguvu ya kisiasa iliyo rasmi.
Rais William Ruto, alipokuwa akizungumza katika ziara yake kaunti ya Nakuru wiki iliyopita, alirejelea maandamano hayo kwa kejeli, akisema:“Mnakumbuka watu walikuwa barabaraniNairobi wamevaa sufuria vichwani, siku hizi wamepotea kwa sababu sasa mnalima chakula,” alisema Rais Ruto.
Kauli hiyo, ingawa ilikuwa ya kufurahisha, ilifufua kumbukumbu za “Vuguvugu la Sufuria” — na sasa, kwa ombi hili jipya la chama, ishara hiyo imepata uhai upya katika kamusi ya kisiasa ya Kenya.
Wakati wa maandamano hayo, wafuasi wa upinzani walijitokeza kila Jumatatu na Alhamisi wakiwa wamevaa sufuria vichwani, wakipiga kelele na kuimba kuhusu njaa na ugumu wa maisha. Picha hizo zilienea kote nchini zikionyesha hali ngumu ya wananchi kutokana na bei ya juu ya vyakula na mafuta.
Ingawa maandamano hayo yaliisha baada ya mazungumzo na hatua kali za usalama, urithi wake umeendelea — si tu kupitia nyimbo na vibonzo, bali sasa pia kupitia jaribio la kusajili chama kinachotumia alama hiyo ya sufuria.
Kenya kwa sasa ina zaidi ya vyama 80 vilivyosajiliwa, lakini vingi havina ushawishi mkubwa. Hata hivyo, wachambuzi wanaamini kuwa alama ya sufuria inaweza kupatia KGP umaarufu wa kipekee, hasa miongoni mwa vijana na wapiga kura wa mijini waliochoshwa na siasa za kawaida.