Fumbo la mshukiwa wa mauaji KNH Kalombotole
MSHUKIWA wa mauaji ya wagonjwa wawili katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) anasalia kuwa kitendawili kwa taifa, si tu baada ya jina lake Kennedy Kalombotole kuibuka, bali pia baada ya upekuzi kubaini sehemu ya utambulisho wake.
Alhamisi iliyopita, hakimu wa Mahakama ya Kibera Daisy Mutai alikiri kutatizika na fumbo linalomzingira Kalombotole.
“Ni vigumu hata kumuachilia mshukiwa kwa dhamana kwa sababu utambulisho wake wa kweli haujulikani. Mshukiwa hana makazi na familia yake haijabainika kwa hivyo kuhitimisha mchakato huu kutakuwa kugumu,” akasema Bi Mutai alipotoa uamuzi Kalombotole azuiwe katika Hospitali ya Mbagathi chini ya uangalizi mkali wa polisi.
Mahakama ilipokea ripoti ya hali ya afya ya Bw Kalombotole ikiambiwa mshukiwa anaugua kisukari na kifafa kwa hivyo alihitajika kuondolewa katika kizuizi cha Kituo cha Polisi cha Kilimani na kuhamishiwa hospitalini ili apokee matibabu ipasavyo.
Lakini katika mahojiano yetu na mmoja wa mawakili wake, ambaye jina lake tunalibana kwa sababu ya mchakato wa kisheria, sehemu ya fumbo hilo ilitatuliwa.
“Mteja wangu anaitwa Peter na jina la Kennedy Kalombotole haliwakilishi mteja wangu. Hana makazi ya kudumu, amelelewa mitaani na mama yake mzazi alifariki dunia miaka kadhaa iliyopita,” akasema.
Anaongeza kuwa mteja wake ni mtu kutoka mojawapo ya makabila ya Kenya na lafudhi (lugha) yake inapatikana Kenya wala si raia wa kigeni jinsi wengi wanavyofikiria.
“Ni jambo la kushangaza kuona serikali ikisukuma kesi dhidi ya mtu ambaye haijamtambua rasmi. Hata mahakama imekiri hivyo,” anasema.
Kwa mujibu wa wakili huyo, taarifa zilizopo ni kuwa kuna faili mbili ya kijamii katika hopitali ya KNH yenye historia ya mshukiwa, lakini hajawahi kupewa nakala hizo licha ya kuomba.
“Niliambiwa mmoja wa maafisa KNH aliyejaribu kunisaidia alionywa kuwa anaweza kufutwa kazi kwa kuzungumza nami kuhusu Kalombotole,” akafichua.
Mara ya kwanza mshukiwa alipokewa hospitalini ni Novemba 2022, na jina lake la Kalombotole likatumika kufungua faili ya mgonjwa.
Katika tukio hilo, mshukiwa alikuwa amelazwa hospitalini humo kama mgonjwa, lakini hakuna stakabadhi za utambulisho zilizowahi kuambatishwa.
Uchunguzi wa ndani haukuwahi kufichuliwa, na mshukiwa aliendelea kulazwa kama mgonjwa wa kawaida hadi tukio la pili la mauaji mwezi Julai 2025.
Tukio la pili lilihusisha kifo cha mgonjwa mwingine katika wadi hiyo hiyo, tukio lililozua maswali zaidi kuhusu usalama wa wagonjwa na mienendo ya mshukiwa ndani ya hospitali hiyo.
Wapelelezi wa jinai wamekiri kwamba bado hawana nyaraka za kuuthibitisha rasmi utambulisho wa Kalombotole, lakini wameahidi kuwasilisha ripoti ya uchunguzi wa kiakili na kijamii kwa haraka.
Huku hayo yakijiri, Mahakama ya Kibera Alhamisi iliamuru mshukiwa azuiliwe kwa muda wa siku 10 katika Hospitali ya Mbagathi akisubiri tathmini ya afya ya akili.
Wakati huo huo, maombi ya Mbagathi kupinga uamuzi huo yamewasilishwa, wakieleza kuwa wadi za wanaume zimejaa na hawawezi kumpokea mshukiwa.
Mnamo Jumanne, Jaji wa Mahakama ya Kibera Diana Kavedza aliamuru Bw Kalombotole ahamishwe kwenda rumande ya gereza la Industrial Area akisubiri vipimo vya hali ya akili ambapo anaendelea kupokea matibabu chini ya uangalizi.
Kwa sasa, taifa linabaki na maswali: Kalombotole ni nani hasa? Na je, anahusika kweli na mauaji ya wagonjwa wawili, au kuna fumbo kubwa zaidi nyuma ya sura yake?