Habari

Fumbo la ndege ya Kenya kupiga abautani TZ

July 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

NDEGE iliyokuwa ikisafirisha wajumbe wa Rais Uhuru Kenyatta katika mazishi ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Benjamin Mkapa, Jumanne ilirudi nchini ghafla na kuibua maswali kuhusu uhusiano wa mataifa hayo mawili jirani.

Ujumbe huo uliokuwa ukiongozwa na Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Bw Samuel Poghisio, haukufanikiwa kuwasili Dar es Salaam kwa kuwa ndege yao ilibadili mwendo ilipofika eneo la Monduli.

Eneo hilo ni takriban kilomita 670 kutoka Dar es Salaam na takriban kilomita 300 kutoka Nairobi.

“Tulikuwa tunategemea ujio wa mjumbe maalum wa Rais wa Kenya lakini tumepata taarifa muda mfupi uliopita kuwa ndege yake imelazimika kurudi Kenya alipofika Monduli na wanaelekea kufika Nairobi salama,” alitangaza Waziri wa Mashauri ya Kigeni na Ushirikiano Afrika Mashariki wa nchini Tanzania, Prof Palamagamba Kabudi.

Tukio hilo liliibua maswali miongoni mwa Wakenya wengi, kwani mnamo Jumatatu, Rais Kenyatta alikuwa amekashifu mataifa ambayo alidai yanaficha ukweli kuhusu janga la corona.

Ingawa hakutaja nchi yoyote, matamshi ya Rais yalichukuliwa na baadhi ya wadadisi kwamba yalielekezwa kwa nchi jirani ya Tanzania, ambapo Rais John Pombe Magufuli analaumiwa kimataifa kwa kutolichukulia janga hilo kwa uzito.

“Tusijilinganishe na wengine kwa kusema huko kwingine hakuna (corona). Nakumbusha Wakenya tunaishi kwa nchi ambayo ina demokrasia, nchi ambayo ina uhuru wa wanahabari. Sisi kama taifa, hatuna nguvu ya kuficha chochote. Yale ambayo yanatendendeka, tunawaambia. Tunajivunia uwezo wa kuambiana ukweli badala ya kuficha kisha wananchi wetu wateseke kimyakimya,” Rais Kenyatta alisema alipohutubu Jumatatu.

Nchini Tanzania, shughuli nyingi za kawaida zinaendelea, kinyume na ilivyo katika mataifa mengine ulimwenguni ambapo zimekwama kwa sababu maambukizi yanaongezeka kwa kasi.

Serikali ya Tanzania iliacha kutangaza idadi ya wagonjwa, huku Dkt Magufuli akihimiza wananchi watumie mitishamba kujifukiza wanaposhuku wameambukizwa, na si lazima kwa wenyeji kuvalia barakoa huku mikusanyiko ya hadhara pia ikiendelea bila tatizo.

Wakati Prof Kabudi alieleza kwamba ndege ya wajumbe wa Kenya haikuwasili, aliongeza kwamba pia wajumbe wa Zimbabwe hawakufanikiwa kufika.

Walikuwa wametarajiwa kuhudhuria hafla ya kumuaga Mkapa katika uwanja wa michezo wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni nchini ilitarajiwa kutoa taarifa rasmi kuhusu tukio hilo lisilo la kawaida lakini haikuwa imefanya hivyo kufikia wakati wa gazeti hili kuchapishwa.

Duru zilisema Bw Poghisio na wenzake walilazimika kurudi kwa sababu ya hali mbaya ya hewa, Hiyo ndiyo sababu iliyotolewa na wajumbe kutoka Zimbabwe.

Hata hivyo, upekuzi wa Taifa Leo ulionyesha kwamba, hali ya hewa ilikuwa shwari katika eneo la Monduli jana Jumanne kwani jua lilikuwa liimeangaza vyema, hapakuwa na upepo mkali na kiwango cha joto kilikuwa nyuzi 21.

Marehemu Mkapa ambaye aliongoza Tanzania kuanzia 1995 hadi 2005 alifariki Alhamisi iliyopita akiwa na umri wa miaka 81.

Familia yake ilisema alikuwa akiugua malaria, akafariki kwa mshtuko wa moyo. Mwili wake ulipelekwa katika kijiji chake cha Lupaso, Wilaya ya Masasi eneo la Mtwara ambapo anatarajiwa kuzikwa leo Jumatano.