Furaha Katibu wa Msikiti wa Jamia akipewa tuzo ya hadhi ya Mashujaa
BARAZA la Kitaifa la Kuwatambua na Kuwatuza Mashujaa, limesema kuwa huwa linazingatia maadili na mchango wa mtu kwa kushirikiana na asasi mbalimbali na wanaostahili ndio hutuzwa.
Afisa Mkuu Mtendaji, Bw Charles Wambia, amesema wao hufanya kazi na mashirika kadhaa ikiwemo serikali za kaunti kuwasaka mashujaa na wale ambao wana mchango wa kuridhisha ndio huunda orodha inayotolewa na serikali.
Katika kuwasaka na kuwatambua mashujaa, wao hushirikiana na Baraza la Magavana (COG) na Makamishina wa kaunti.
“Tangu baraza hili libuniwe miaka mitatu iliyopita, tumezama na kuwatuza tu wale ambao hufanya kazi nzuri hata katika kaunti zao,” akasema Bw Wambia.
Alikuwa akiongea Jumanne katika Msikiti wa Jamia alipomtuza Katibu wa Msikiti Abdulbari Hamid, cheti cha kutambuliwa, medali na hadhi kutoka kwa Rais William Ruto.
Bw Hamid alikuwa kati ya vigogo ambao walitambuliwa kwenye orodha ya Siku ya Mashujaa katika Kaunti ya Kitui mnamo Oktoba 20.
Alijizolea hadhi hiyo kutokana na kazi na miradi anayoshiriki ya kuinua wasiojiweza katika jamii.

Shughuli hiyo pia ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Msikiti wa Jamia Osman Warfa, Imam Jamaldin Osman pamoja na viongozi wengine wa kidini na wa Kiislamu.
Tuzo hiyo ilitolewa wakati ambapo msikiti huo nao unaendelea na maadhimisho ya miaka 100 tangu ujengwe.

“Nataka nishukuru baraza hili kwa kunitunuku na pia wafanyakazi katika msikiti huu ambao wamechangia nituzwe. Hii inaonyesha kuwa hatutimizi tu mahitaji ya kidini bali pia misaada ya kuwainua wenzetu wasiojaliwa katika jamii,” akasema Bw Hamid.
Bw Warfa alisema tuzo hiyo inaonyesha kuwa hata maeneo ya kuabudu kama misikiti hutambuliwa kutokana na miradi wanayoshiriki