Furaha vijana 200 wakisajiliwa kusomea kozi za kiufundi Migori
ZAIDI ya vijana 200 kutoka Kaunti ya Migori sasa wanaweza kupokea mafunzo ya kazi za mikono baada ya kusajiliwa kusomea kozi za kiufundi.
Haya yanakuja wakati ambapo shirika moja lisilo la kiserikali limekarabati na kuchimba mabwawa 23 katika kaunti hiyo ili kuwapa wakazi maji.
Shining Hopes for Communities (SHOFCO) imewasajili vijana 200 kwenye mpango huo wa mafunzo ambapo watasomeshwa ushonaji nguo, kazi za umekanika, teknolojia na ujenzi ili kuwasaidia kujikimu.
Isitoshe, zaidi ya vijana 2,000 wamepokea mtaji wa kuwasaidia kuanzisha biashara zao ili kupambana na ukosefu wa ajira na kuwawezesha kuwa wavumbuzi.
“Mabadiliko yanaanza wakati ambapo jamii inaamua mustakabali wake. Hapa Migori tunawaona watu wakikumbatia miradi ambayo itaamua mustakabali wao,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa Shofco Kennedy Odede akiwa Migori.
Ujenzi wa mabwawa 23 maeneo mbalimbali Kaunti ya Migori kutasaidia raia wanapata maji safi, wanashiriki kilimo cha unyunyuziaji mashamba maji na pia ufugaji wa samaki.
Bw Odede pia alitangaza kuwa kuna mpango wa kuwasaidia vijana 1000 Migori kuanzisha biashara mnamo 2026.
Naibu Gavana wa Migori Joseph Mahiri, aliyekuwa Mbunge wa Rarieda Nicholas Gumbo na Kiongozi wa Wengi Kaunti ya Migori Edward Ooro wote walisifu mipango ambayo imekuwa ikiendeshwa na Shofco kusaidia kupambana na umaskini kote nchini.
“Kwa ushirikiano, tunatoa jukwaa bora la maendeleo ambalo limebuniwa na raia wenyewe,” akasema Bw Mahiri.
Bw Ouma naye aliwaomba vijana wasisubiri nafasi za kazi lakini wazibuni ili wajitegemee.
“Familia nyingi zitakuwa zikijiweza kiuchumi iwapo vijana watatumia vyema nafasi ambazo wanapata,” akasema Bw Ooro.
Bw Gumbo naye alisema baadhi ya miradi iliyoanzishwa na Shofco na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali, inaashiria ari ya kuhakikisha kuwa wanajitegemea.