Habari

Gachagua aendelea kuikosoa miradi ya Ruto akidai ni feki

Na WAIKWA MAINA April 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ALIYEKUWA Naibu Rais, Rigathi Gachagua, ameendelea kumshutumu Rais William Ruto, akidai kuwa miradi mingi anayozindua ni ya kisiasa tu na si ya kutekelezwa.

Bw Gachagua alidai kuwa alipokuwa Naibu Rais, aligundua kuwa kuzindua miradi mingi hakumaanishi kuwa itatekelezwa.

Kuna wakati tulizindua ujenzi wa barabara ya Boiman, lakini muda mfupi baadaye niliarifiwa kuwa mwanakandarasi aliondoka mara tu baada ya Rais kuondoka. Nilipomwambia Rais, alionekana kucheka na hakujali. Aliniambia kuwa kuzindua miradi ni siasa, na si lazima ahadi zote zitimizwe —  Bw Gachagua

Gachagua alijuta kuwa aliwapotosha Wakenya kuhusu Rais wakati wa kampeni.

“Nakubali nilikosea, nilidanganywa. Kama aliweza kuwadanganya maaskofu, je, mtu kama Rigathi ni nani? Najuta na naomba msamaha kwa yale niliyosema kuhusu Rais wa zamani Uhuru Kenyatta.”

Alizungumza kwenye harambee katika Kanisa la St Louis Igwamiti Catholic Church Kaunti ya Nyandarua, ambapo hakuna mwanasiasa aliyetangaza mchango wake hadharani.

Alidai kuwa Rais ametembelea Nyandarua mara tisa, kila mara akiahidi miradi ya maendeleo ambayo haijatimizwa.

“Tulipozindua Barabara ya Boiman, MCA wa eneo hilo aliniita muda mfupi baadaye akisema mwanakandarasi aliondoka mara tu baada ya helikopta ya Rais kupaa. Nilipomjulisha Rais, alicheka na kusema kuwa hizo ni ‘siasa’. Hii nchi inaharibiwa na uongo wa viongozi wa juu,” alisema Gachagua akisisitiza kanisa ndilo limebaki kuwa sauti ya kutetea Wakenya baada ya Bunge na Seneti ‘kununuliwa’ na serikali.