Habari

Gachagua akatiza ziara yake ya miezi 2 Amerika kushirika kampeni za chaguzi ndogo

Na CHARLES WASONGA August 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua amekatiza ziara yake nchini Amerika ili arejee nyumbani kujishughulisha na kampeni za chaguzi ndogo zijazo.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) tayari imetangaza kuwa chaguzi hizo zote 23 zitafanyika Novemba 27, mwaka huu.

Hata hivyo, kipindi rasmi cha kampeni ni kuanzia Oktoba 8, 2025 hadi Novemba 24, 2025.

Kwenye taarifa aliyoitoa Alhamisi, Agosti 14, 2025, Gachagua aliwaomba radhi Wakenya walioko Amerika akisema hangeweza kuwatembelea katika majimbo mengi alivyopanga.

“Ziara yangu nchini Amerika imefana zaidi kwani nimepata fursa ya kufanya mazungumzo na Wakenya katikka majimbo mengi,” akasema.

“Hata hivyo, nawaomba radhi waandalizi wa ziara hiyo na Wakenya kuwa sitaweza kuzuru majimbo zaidi kwani nahitaji kurejea nyumbani kushirikiana na maafisa wa chama chetu cha DCP katika matayarisho ya chaguzi ndogo zijazo katika sehemu mbalimbali za nchini,” Bw Gachagua akaongeza.

Bw Gachagua alifichua kuwa amerejelea shughuli zake Amerika mapema mwaka ujao, akisema kuwa ratiba yake itatolewa kwa umma.

Aidha, kiongozi huyo wa DCP alisema atapumzika kwa siku kadhaa kabla ya kuanza safari ya kurejea Kenya akiandamana na mkewe, Pasta Dorcas.

Bw Gachagua amewashukuru Wakenya wanaoishi Amerika kwa kumpa mapokezi mazuri alipotua nchini humo Julai 9.

“Aidha, nawahongera waandalizi na maafisa wa chama cha DCP matawi ya majimbo mbalimbali kwa mipango mizuri na ushirikishi mzuri. Mlifanya kazi nzuri,” akasema.

Baadhi ya maeneo wakilishi ambako IEBC itaandaa chaguzi ndogo ni kaunti ya Baringo (kiti cha useneta) na maeneo bunge ya Banissa, Magarini, Kasipul, Ugunja, Mbeere Kaskazini na Malava.

Aidha, itaendesha chaguzi ndogo katika wadi 16 zilizoko maeneo mbalimbali nchini.

Naibu Kiongozi wa DCP Cleophas Malala ametangaza kuwa chama hicho kitadhamini wagombeaji katika maeneo yote wakilishi yaliyoko wazi.

“Tayari tumemtaja Edgar Busiega atakayepeperusha bendera yetu katika uchaguzi mdogo katika eneo bunge la Malava huku Aden Mohamed akiwa mgombeaji wetu katika eneo bunge la Banissa.

Wadadisi wanasema kuwa chaguzi hizo ndogo ni mtihani mkubwa wa Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga wanaoshirikiana katika serikali jumuishi.

“Matokeo yake yatatoa kiashirio kuhusu hali itakavyokuwa katika uchaguzi mkuu wa 2027. Ikiwa Rais Ruto na mshirika wake, Raila Odinga, watasalia uongozini au la. Upinzani nao utajipima kubaini ikiwa unaweza kushirikiana na kufaulu kumwangusha au la,” anasema Bw Martin Andati.