Gachagua arejea kuokoa Upinzani uliotolewa pumzi na serikali
KIONGOZI wa Chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) Rigathi Gachagua amekatiza ziara yake ya kisiasa nchini Amerika kuokoa upinzani unaoonekana kufifia.
Ingawa mbunge wa Kapseret Oscar Sudi anadai kuwa “Kenya ilishinikiza Amerika kukatiza ziara hiyo,” Bw Gachagua amesema aliamua kivyake kurejea nyumbani.
Bw Gachagua aliondoka nchini mnamo Julai 9 kwa kile alichokitaja kuwa ni ziara ya miezi miwili Amerika.
Aliratibiwa kurejea Kenya mnamo Septemba 8, 2025 lakini sasa anadai kurejea nyumbani mapema “kuongoza kampeni za chaguzi ndogo zijazo.”
Kwenye ujumbe aliyoweka kwenye ukurasa wake wa Facebook jana, Bw Gachagua alisema ziara yake ilikuwa yenye fanaka kwani ‘nilifanya majadiliano mazito na Wakenya ughaibuni.’
Akiwa Amerika, Bw Gachagua amekuwa akiikosoa serikali ya Rais William Ruto akiihusisha na maovu kama vile ugaidi, ufisadi na ukiukaji wa haki za kibinadamu.
Aidha, alionya serikali ya Dkt Ruto dhidi ya kujaribu kuiba kura za urais katika uchaguzi mkuu ujao akidai hatua hiyo inaweza kuchochea ghasia.
Tangu alipoondoka nchini, vinara wenzake wa upinzani wameshindwa kuendeleza kasi ya kuikosoa serikali.
Imekuwa nadra kwa vinara hao kama vile Kalonzo Musyoka (Wiper), Martha Karua (PLP), Eugene Wamalwa (PLP) na aliyekuwa Waziri wa Usalama Fred Matiang’i kuitisha vikao vya wanahabari kuikosoa serikali.
Suala la upinzani kuwa “baridi” bila Gachagua juzi liliangaziwa na Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni.
Aidha, wafuasi wake kama vile Maseneta Joe Nyutu (Murang’a), John Methu (Nyandarua), Karungu Thang’wah (Kiambu) na wengine wamekuwa wakishambuliwa na polisi kila wakijaribu kuwahutubia raia.
Jana, Bw Gachagua alisikitika kuwa anarejea Kenya bila kutembelea baadhi ya majimbo ya Amerika.
“Nasikitika kuwa sitaweza kukutana na Wakenya katika majimbo mengine ilivyopangwa. Hii ni kwa sababu ninahitaji kurejea nyumbani kuungana na viongozi wa chama chetu, DCP, kwa matayarisho ya chaguzi ndogo zijazo,” akasema.
Hata hivyo, kipindi rasmi cha kampeni hizo ni kuanzia Oktoba 8 hadi Novemba 24, 2025.
Wiki jana, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilitangaza kuwa chaguzi hizo zote 23 zitafanyika Novemba 27, mwaka huu.
Baadhi ya maeneo wakilishi ambako IEBC itaandaa chaguzi ndogo ni kaunti ya Baringo (kiti cha useneta) na maeneo bunge ya Banissa, Magarini, Kasipul, Ugunja, Mbeere Kaskazini na Malava.
Aidha, itaendesha chaguzi ndogo katika wadi 16 zilizoko maeneo mbalimbali nchini.
Naibu Kiongozi wa DCP Cleophas Malala ametangaza kuwa chama hicho kitadhamini wagombeaji katika maeneo yote wakilishi yaliyoko wazi.
“Tayari tumemtaja Edgar Busiega atakayepeperusha bendera yetu Malava huku Aden Mohamed akiwa mgombeaji wetu Banissa.”
Hata hivyo, uchaguzi mdogo wenye umuhimu mkubwa kwa Bw Gachagua na upinzani ule wa eneobunge la Mbeere Kaskazini, ulioko eneo la Mlima Kenya Mashariki.
Anapania kuutumia kumdhihirishia Rais Ruto kwamba ametwaa udhibiti, kisiasa, wa eneo pana la Mlima Kenya na kwamba kiongozi wa taifa atapoteza jumla ya kura 3.5 milioni za eneo hilo 2027.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa DCP Cleophas Malala jana alitoa taarifa akidai serikali inapanga njama ya kumkamata Bw Gachagua atakapowasili nchini kutoka Amerika.
Hata hivyo, Seneta huyo wa zamani wa Kakamega hakutoa maelezo zaidi kuhusu madai hayo.