Habari

Gachagua atua Kirinyaga, adai Waiguru alilipa wanawake kuandamana kwa kumkosoa

Na GEORGE MUNENE October 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua alirejea katika Kaunti ya Kirinyaga Jumanne na kumshambulia vikali Gavana Anne Waiguru, akimlaumu kwa kuandaa maandamano dhidi yake.

Gachagua alidai kuwa Waiguru aliwakusanya wanawake wachache kutoka eneo hilo ili waandamane dhidi yake kwa sababu ya matamshi aliyotoa kumhusu.

“Waiguru aliandaa wanawake wachache kunipigia kelele kwa kusema ukweli kumhusu. Lazima aondoke,” alisema Gachagua mjini Ngurubani huku akishangiliwa.

Gachagua alisisitiza kuwa ataendelea kuwafichua viongozi kutoka Mlima Kenya ambao anadai wanashirikiana na Rais William Ruto kuleta mgawanyiko katika eneo hilo.

“Waiguru alikasirika nilipomwanika. Kiongozi yeyote wa hapa anayeshirikiana na Rais Ruto ni adui wa Mlima Kenya,” alisema Gachagua.

Alimtaja Waiguru na viongozi wa eneo hilo wanaoegemea upande wa Rais Ruto kuwa ni wasaliti wasiostahili kuongoza.

“Wakati mchele wa bei nafuu uliingizwa nchini, Waiguru hakufanya maandamano. Lakini nilipomwambia anawasaliti watu wetu, akawatuma wanawake barabarani. Ni jambo la kusikitisha,” alisema.

Gachagua aliwataka wakazi wa Kirinyaga kupiga kura kutimua wabunge wa eneo hilo wanaohusishwa na Rais Ruto wakiwemo Mary Maingi (Mwea), Gichimu Githinji (Gichugu), na George Kariuki (Ndia).

“Wabunge hawa pia ni maadui wetu na lazima waondoke,” alisisitiza.

Seneta wa Kirinyaga Kamau Murango naye aliungana naye akilaani matumizi ya wanawake katika maandamano dhidi ya Gachagua.

“Waiguru anawatumia wanawake wa Kirinyaga vibaya. Aache mara moja,” alisema Murango.

Gachagua alitoa wito kwa wakaazi wa Mlima Kenya kudumisha umoja na kupinga njama zozote za kuwatenganisha.

Siku ya Jumatatu, mamia ya wanawake waliandamana katika mji wa Kutus wakilalamikia matusi na dharau ambazo Gachagua amekuwa akimwelekezea  Gavana Waiguru.

Wakiwa na mabango, wanawake hao waliandamana asubuhi nzima na kumtaka Gachagua kuacha kuvunjia heshima kiongozi wao.
Waliziba sehemu ya barabara kuu ya Kutus–Embu, wakawasha matairi, na kusababisha msongamano mkubwa wa magari.

Maafisa wa polisi waliovaa kiraia walifuatilia maandamano hayo kwa mbali bila kuingilia.

“Sisi kama wanawake wa Kirinyaga tumechoshwa na Gachagua. Aache kumkosea heshima Gavana wetu Waiguru,” alisema Bi Wanjiru Wanjohi.

Walisisitiza kuwa walimchagua Waiguru kwa hiari na hivyo anapaswa kuheshimiwa kama kiongozi wao halali.