Habari

Gachagua, Kindiki wakabana koo Mbeere wananchi wakilia kupuuzwa

Na CECIL ODONGO November 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UCHAGUZI wa Novemba 27 wa Mbeere Kaskazini sasa umegeuka vita vya ubabe huku viongozi wakionyesha ukwasi kwa kuchapa kampeni kali kuwavumisha wagombeaji wao.

Sehemu kubwa ya eneobunge la Mbeere Kaskazini ni kame lakini upinzani na serikali unaendelea kutifuana huku wananchi wenyewe wakiwa mashabiki licha ya hali ngumu ya maisha.

Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki, Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku na Gavana wa Embu Cecily Mbarire wanakabaliana na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Mbunge wa Manyatta Gitonga Mukunji na Mwanasheria Mkuu Justin Muturi miongoni mwa wengine.

Mirengo yote miwili inapambana kuonyesha ushawishi wao huku wawaniaji wanaogombea wakionekana kuzamishwa kwenye mashindano ya ubabe kati ya Prof Kindiki na Bw Gachagua.

Mtihani wa kushinda kiti hicho utaonyesha iwapo ni Prof Kindiki au Bw Gachagua ndiye mbabe wa siasa za Mlima Kenya.

Prof Kindiki anamuunga mkono Leonard Muthende wa UDA naye Bw Gachagua yupo nyuma ya Kiongozi wa DP Newton Kariuki maarufu kama Newton Karish.

Wakati wa mikutano yao ya kisiasa, wawili hao wamekuwa wakikashifiana hadharani.

Mnamo Jumatatu Prof Kindiki aliwaambia wakazi wa Soko la Ishiara kwamba yeye ndiye kigogo wa siasa za Ukanda wa Mlima Kenya wala si Bw Gachagua.

“Nani alimchagua kigogo wa siasa za Mlima Kenya? Mimi ndiye mfalme wa mlima nikiwa na uzoefu wa miaka 20 kama kiongozi aliyechaguliwa. Pia niliwakilisha Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta katika Mahakama ya ICC na Rais William Ruto,” akasema Prof Kindiki.

“Huyo jamaa amekuwa akijigamba yeye ndiye mfalme ilhali sisi ndio tunapigania miradi ya maendeleo. Alikuwa mamlakani lakini hakufanya chochote kuimarisha maisha ya watu wa eneo hili,” akaongeza.

Naibu Rais alisema kuwa atakita kambi Mbeere Kaskazini hadi uchaguzi huo mdogo ukamilike kisha ampeleke Bw Muthende bungeni aapishwe na Ikulu akutane na Rais Ruto.

Bw Gachagua naye amekuwa akiendesha kampeni ya nyumba hadi nyumba huku akiwataka wakazi wasimchague mradi wa serikali.

“Wanatumia pesa nyingi kuwalazimishia mwaniaji wao. Chukueni pesa lakini kura mpige kwa hekima,” akasema akiwa katika Kituo cha Kibiashara cha Kamumu mnamo Jumatano Novemba 19, 2025.

Huku mibabe wa kisiasa wakitifuana, wakazi nao wanasema changamoto wanazokabiliana nazo zimekuwa zikipuuzwa. Barabara mbovu, ukosefu wa maji safi, umeme kupotea mara kwa mara na maeneo mengi kutounganishiwa umeme ni kati ya masuala ambayo wanalalamikia hayajatatuliwa.