Gachagua: Mimi ndiye niko pazuri zaidi kumfanya Ruto wantam
ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua anajaribu kurejea tena kwenye siasa kwa kishindo, safari ambayo sasa inajumuisha azma ya kuwania urais, hatua ambayo wachanganuzi wanatafsiri kama mbinu ya kiakili au kosa kubwa litakalofifisha kabisa maisha yake ya kisiasa.
Kwa baadhi ya watu, wazo la Bw Gachagua kuwa rais ni jambo lisilowezekana, hasa kwa kuwa ana doa la kufurushwa kwa njia ya kuondolewa madarakani.
Hata hivyo, wengine wanahisi ni mapema mno kumpuuza.
Wafuasi wake huelezea mikakati yake kama mchezo wa saratanji (chess) wa kiwango cha juu.
Lakini, hata mchezo huo wa heshima una kanuni na taratibu zinazotabirika.
Wengi walimwona Bw Gachagua kama anayeweza kutoa mwelekeo katika upinzani.
Lakini sasa anasema yeye ndiye anayefaa zaidi kukabiliana ana kwa ana na Rais William Ruto katika uchaguzi wa 2027, msimamo ambao tayari umewatia kiwewe washirika wake ndani ya muungano huo wa upinzani.
“Naomba mnisaidie katika azma yangu ya kuwania urais ili nimpeleke Ruto nyumbani. Alitudanganya tuingie kwenye harusi (uchaguzi) kwa farasi wa kukodi (bila chama chetu), lakini sasa tunaelewa,” alisema Bw Gachagua Jumapili alipohutubu katika Kaunti ya Nyandarua.
Hii si mara ya kwanza kwa Bw Gachagua kueleza msimamo kama huo lakini sasa inadhihirika kuwa alikuwa na mpango maalum.
“Ninaamini mimi ndiye bora zaidi na ninapaswa kuwa mgombea wa upande wetu. Iwapo hilo halitatimia na mtu mwingine achaguliwe, nimesema nitamuunga mkono,” alitangaza miezi mitatu iliyopita wakati wa kuzindua chama chake cha Democratic Change Party (DCP).
Wachambuzi wanasema Bw Gachagua anajaribu kufikiria hatua kumi mbele huku wengine wakijikokota kupanga hatua ya pili.
Je, hili linamfanya kuwa kiongozi mwenye maono ya mbali, au mtu ambaye amepotea katika hali halisi ya siasa za Kenya?
Hilo ndilo swali kuu linalotawala mijadala ya kisiasa sasa.
Hata hivyo, mawakili wa Bw Gachagua wanasema kwa kuwa amepinga kesi hiyo ya kuondolewa kwake mahakamani, uamuzi wa kutofaa kwake kushikilia wadhifa wa serikali umesitishwa hadi uamuzi wa mwisho wa mahakama utakapotolewa.
Wananukuu uamuzi wa Mahakama ya Juu katika kesi ya aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Mike Sonko, ambapo iliamuliwa kuwa marufuku ya kushika wadhifa wa umma huanza tu baada ya kukamilika kwa rufaa zote za kisheria.
Kwa msingi huo, wanaamini Bw Gachagua ana nafasi tatu za kuhakikisha anaruhusiwa na Tume ya Uchaguzi kuwania iwapo atataka: Kugeuza uamuzi wa Seneti mahakamani kwa hoja kwamba aliondolewa kwa misingi ya kisiasa, si ukiukaji wa Sura ya Sita ya Katiba, kupata amri ya muda ya mahakama kusitisha athari za kufutwa kwake hadi kesi itakaposikilizwa kikamilifu kushawishi mahakama kutamka kuwa kuondolewa kwake kulikuwa kuwindwa kisiasa, na hivyo kifungu cha 75(3) cha Katiba hakifai kutumika kwake.
Waziri wa zamani wa Kilimo, Bw Mithika Linturi, anaunga mkono msimamo wa mawakili wa Bw Gachagua.
Lakini Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni, hakubaliani naye: “Elimu ya uraia itawasaidia wananchi kuelewa maana ya kuondolewa ofisini chini ya Katiba ya 2010,” alisema.
Katika ngome yake ya Mlima Kenya, hali ni tata zaidi. Bw Gachagua anapendwa kama sauti kali ya upinzani, lakini wengi wanamtilia shaka kama kiongozi wa kitaifa.
“Wanataka amkosoe Ruto, lakini si kuchukua usukani,” alisema mmoja wa wasaidizi wake.
“Ukiwauliza kati ya Gachagua na William, watu wa mlima watasema wanataka ‘Tutam’ (mihula miwili), si ‘Wantam’ (muhula mmoja),” aliongeza mwingine.
Kwa wanaofuatilia historia ya siasa za Kenya, tukio la mwaka 1966 halikwepeki – pale Jaramogi Odinga alipovunja uhusiano na Jomo Kenyatta, na akatengwa kabisa kisiasa licha ya kupendwa na wafuasi wake.
Hatari kwa Gachagua si tu kutoka kwa ngome yake.
Iwapo atasisitiza kuwania, atajikuta kwenye uwanja uliojaa wapinzani – akiwemo Prof Kindiki anayewakilisha mfumo uliopo, Martha Karua anayeaminika kwa mwelekeo wa mageuzi, na Moses Kuria ambaye ni mtaalamu wa kuchochea na mbinu kali.