Gachagua: Uchaguzi 2027 nitakuwa ndani kabisa
ALIYEKUWA naibu rais, Rigathi Gachagua, amesema atawania urais mwaka wa 2027 kwa lengo la kumng’oa Rais William Ruto mamlakani.
Bw Gachagua, ambaye anatarajiwa kuzindua chama chake cha kisiasa mwezi ujao, hata hivyo aliongeza kwa haraka kuwa yuko tayari kumuunga mkono mgombea mwingine maarufu zaidi “ili kumfanya Dkt Ruto kuwa rais wa muhula mmoja tu”.
Alisema kuwa chama chake pia kitalenga kuwaondoa wabunge wote wanaounga mkono Rais Ruto.
Akifichua kuwa aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mithika Linturi, atashikilia wadhifa wa juu katika chama hicho, Bw Gachagua alisema anashirikiana kwa karibu na viongozi wa vyama vingine vya upinzani kuunda mkakati wa kupata zaidi ya asilimia 70 ya kura ili kumshinda Dkt Ruto katika duru ya kwanza ya uchaguzi.
Alizungumza hayo usiku wa Jumapili katika mahojiano na runinga ya Weru inayotangaza kutoka Meru.
“Mradi kesi yangu ya kupinga kuondolewa madarakani haijafika katika Mahakama ya Juu, nitawania urais. Nashirikiana na Kalonzo Musyoka, Martha Karua, Eugene Wamalwa, George Natembeya na Fred Matiang’i kuunda muungano utakaoshinda. Tutazingatia kura kwanza kisha tukubaliane nani atakuwa mgombeaji urais wetu. Nitaachia atakayeungwa na wengi wetu, kwa sababu Ruto lazima aondoke,” alisema Bw Gachagua.
Aliongeza kuwa leo atakutana na viongozi wengine wa vyama kutoka maeneo mbalimbali nchini kupanga namna ya kuunganisha Wakenya dhidi ya Ruto.
Bw Gachagua alisema wanatarajia kutangaza mgombea urais wa upinzani kufikia mwisho wa 2026, na kuongeza kuwa mrengo wake utawekeza kwa utafiti wa kitaalamu kutafuta mbinu ya kumshinda Rais Ruto.
“Tutawashirikisha wataalamu kubuni mkakati sahihi. Tunakusudia kuwa na zaidi ya wabunge 50 kutoka Mlima Kenya. Tunahitaji viongozi wanaotetea maslahi ya wananchi, si maslahi yao ya kibinafsi,” aliongeza.
Akishutumu serikali ya sasa kwa kujihusisha na maslahi ya kibinafsi na kibiashara, Gachagua alisema kipaumbele chao cha kwanza kitakuwa kurejesha heshima ya mshahara.
“Mpango wetu ni kuondoa ushuru wa nyumba nafuu na kukabidhi mpango wa nyumba nafuu kwa kaunti ili wakodishe na kuwalipa Wakenya waliokatwa pesa. Mpango huo ni biashara ya kibinafsi,” alidai.
Aliongeza: “Mpango wetu ni kurejesha demokrasia na utawala wa sheria. Tutaruhusu taasisi kufanya kazi. Serikali yangu itaruhusu baraza la mawaziri kutoa ushauri na kufanya kazi kwa uhuru. Tutawasikiliza wananchi. Kuondolewa kwa Ruto ni lazima ili kuokoa Kenya.”
Akiapa kuendelea kutetea maslahi ya eneo la Mlima Kenya, alilaumu baadhi ya wabunge kwa kuwa waoga na wa kuegemea upande mmoja.
Alisema kuvurugika kwa uhusiano wake na Rais Ruto kulichangiwa na wabunge wa Meru waliokuwa wakimripoti kwa Rais kila alipowataka watetee watu wao.
“Niliwaita wabunge wa Meru kwa mkutano kujadili matatizo tunayopitia na Ruto. Rais alikuwa akiondoa watu wetu serikalini na hivyo niliwashauri tumshinikize atekeleze ahadi zake. Hata hivyo, walinigeuka na kuripoti kwa Rais ambaye alinikasirikia sana,” alisema.
Alidai kuwa biashara ya miraa Somalia imezorota kutokana na kuingiliwa na watu wenye ushawishi serikalini waliovamia sekta hiyo, hali ambayo imesababisha kushuka kwa bei mashambani.
Alimshambulia Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen kwa kutishia kumnyamazisha yeye na aliyekuwa Waziri Justin Muturi kwa kutumia Sheria ya Siri za Serikali.
“Vitisho hivyo ni vya kuchekesha. Tangu lini wizi wa mali ya umma, uhalifu na ufisadi vimekuwa siri za serikali? Tuko tayari kushtakiwa kwa kusema ukweli,” alisema.