Gari la mkopo lamchongea mbunge kampuni ikisaka kibali anyakwe
MBUNGE wa Lamu Magharibi, Bw Stanley Muthama, anakabiliwa na hatari ya kukamatwa kufuatia ombi la mfanyabiashara kwa kushindwa kulipa deni la Sh 7.1 milioni kutokana na ununuzi wa gari karibu miaka tisa iliyopita.
Bi Yvonne Njoki Njiru, anayemiliki kampuni ya Newday Motors Limited, ameomba mahakama kumuamuru Bw Muthama na kampuni yake, Stansha Limited, walipe deni hilo, kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Milimani uliotolewa Aprili 23, 2025.
Hata hivyo, Bw Muthama amekana deni hilo na kudai kuwa haikuwa sawa kwa mahakama kumlazimisha kulipa deni lililohusiana na kampuni ambayo yeye ni mkurugenzi tu.
“Nimehukumiwa kwa deni ambalo si langu bali la kampuni, bila sababu ya msingi. Hali hii inanitia mimi na mali yangu katika hatari,” alisema Bw Muthama katika stakabadhi za mahakama kupinga hatua ya Bi Njiru kutekeleza hukumu hiyo.
Kulingana na stakabadhi za mahakama, deni la awali lilikuwa Sh3.5 milioni kutokana na uuzaji wa gari aina ya Isuzu ELF kwa kampuni ya Stansha Limited mnamo Juni 23, 2016.
Deni hilo limeongezeka hadi Sh7.1 milioni kutokana na riba. Katika maombi yake, Bi Njiru anadai kuwa Bw Muthama aliahidi mara kadhaa kulipa deni hilo lakini hajawahi kutimiza ahadi zake, ikiwemo mnamo Februari 2023 alipokutana naye kwa bahati katika mkahawa mmoja jijini Nairobi.
Anasema kuwa katika mawasiliano yao, Bw Muthama alikiri deni hilo na kuahidi kulipa Sh1 milioni kufikia Desemba 2023. Baada ya kuona hana nia ya kulipa, aliripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Industrial Area, ambapo lilisajiliwa kama OB No. 52/19/10/2023 saa 9:20 alasiri.
Wakili wake, Bw Robinson Kigen, sasa anatekeleza amri ya mahakama na anasisitiza kuwa Bw Muthama ndiye aliyepokea gari hilo.
Alipoulizwa kupitia WhatsApp liko wapi, alijibu kuwa liko Mombasa.
Mahakama ilibaini kuwa Bw Muthama alikiri kuwepo kwa mkataba wa ununuzi wa gari hilo kwa Sh3.5 milioni na alikuwa alipe Sh500,000 kama amana.
Hata hivyo, hakuonyesha ushahidi wowote wa malipo hayo. Hakimu Mkuu H.M Ng’ang’a, alisema kuwa ikiwa Bw Muthama hakuwa sehemu ya mkataba huo, asingefanya ahadi yoyote ya kulipa.
“Mahakama hii inapata kuwa utetezi uliotolewa ni wa kukanusha tu na haufai. Kampuni ya Stansha imekiri kununua gari hilo na haijaonyesha ushahidi wowote wa kulipa. Muthama ndiye alitia saini mkataba huo, bila kuonyesha kuwa alifanya hivyo kama mkurugenzi wa Stansha,” alisema hakimu.
Kesi hiyo itatajwa tena Mei 19, 2025 kusikiliza ombi la kutolewa kibali cha kukamatwa kwa Bw Muthama.
Hatua hii inajiri baada ya Jaji Moses Ado wa Mahakama Kuu kukataa ombi la Bw Muthama la kusimamisha uamuzi wa mahakama ya hakimu hadi rufaa yake isikizwe.
Bw Muthama anasisitiza kuwa hakukuwa na msingi wa yeye kuhusishwa na deni la Stansha Limited.
Anaongeza kuwa Newday Motors walilipwa Sh500,000 na walipaswa kuchukua gari iwapo malipo hayangekamilishwa jambo ambalo hawakufanya.