Habari

Gavana amtetea spika wa bunge la kaunti ya Kiambu

August 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

GAVANA wa Kaunti ya Kiambu Dkt James Nyoro, amesema wale wanaoeneza shinikizo za kutaka spika wa bunge la kaunti Stephen Ndichu atolewe wasahau.

“Kwa wakati huu serikali ya Kaunti ya Kiambu ina mambo mengi ya kutekeleza na kwa hivyo wale wanaosumbuka na siasa ni shauri yao,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema watu wameeneza uvumi usio na msingi kuwa madiwani wa kaunti hii ya Kiambu wanapanga kumng’oa spika wao Stephen Ndichu.

Aidha, alieleza kuwa tayari amekutana na madiwani hao na hakuna jambo kama hilo linalotarajiwa kufanyika wakati wowote ule.

Aliyasema hayo Jumamosi katika hekalu la Visa Oshwal mjini Thika wakati familia 300 zilipewa chakula cha msaada na familia ya Visa Oshwal.

Alisema tayari wanashirikiana na Ujerumani na Amerika ili kupata usaidizi zaidi wa kiafya kutokana wa namna ya kukabiliana na Covid-19.

Alisema hospitali zote kwa sasa zina dawa za kutosha ambapo hakuna mgonjwa yeyote atapata shida ya kukosa dawa iwapo atazuru hospitali katika kaunti hiyo.

Malengo ya Rais

Alisema wakati uliosalia ni mchache mno na kwa hivyo lengo lao kuu litakuwa ni kuendeleza ajenda nne muhimu za serikali ili kufanikisha malengo ya Rais Uhuru Kenyatta.

“Kwa wakati huu cha muhimu kwetu ni kuona ya kwamba miradi yote ambazo hazijakamilika zinaharakishwa ili wananchi wanufaike na huduma wanazopokea.

Mwenyekiti wa shirika la Visa Oshwal Bw Bimal Shah, alisema wataendelea kusaidia walemavu na wasiojiweza ili kuwapa matumaini ya kimaisha.

Watu kutoka kwa familia 300 za kutoka mitaa ya mabanda mjini Thika zilizofaidika kwa kupokea chakula kutoka kwa Visa Oshwal. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema wakati huu wa kusherehekea siku ya Pariashan katika Jamii ya watu wa Bara Asia, ni vyema kuwajali wasio na chochote kama chakula.

Alisema lengo lao ni kuona ya kwamba kila jamii inaishi maisha ya kutamanika na ni sharti kufanya mfungo huku wakizingatia kusameheana.

Alisema familia ya Visa Oshwal imekuwa ikitibu wagonjwa wa macho kila mwaka hapa nchini Kenya kwa zaidi ya miaka 40.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Thika Bw Alfred Wanyoike alisema wafanyabiashara wa Thika wataendelea kushirikiana na familia hiyo ya watu wa Bara Asia kwa lengo la kuleta ushirikiano mzuri kwa wakazi wa eneo hilo.