Gavana Njuki achaguliwa kumrithi Kahiga katika Baraza la Magavana
GAVANA wa Tharaka Nithi Muthomi Njuki amechaguliwa kwa kauli moja kuwa Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG), kumrithi Gavana wa Nyeri, Mutahi Kahiga.
Uchaguzi huo ulifanyika Jumatano wakati wa mkutano wa Baraza lote ulioandaliwa mjini Naivasha, Kaunti ya Nakuru. Mwenyekiti wa CoG ambaye pia ni Gavana wa Wajir, Ahmed Abdullahi, ndiye alitangaza matokeo hayo wakati wa kikao na wanahabari.
Katika taarifa baada ya mkutano huo, Gavana Njuki alishukuru magavana wenzake kwa kumwamini, akitaja uteuzi huo kuwa “heshima kubwa sana.”
“Magavana wenzangu, ninapokea kwa unyenyekevu mkubwa na shukrani tele imani mliyoonyesha kwangu. Naahidi kulinda hadhi ya ofisi hii na kushirikiana nanyi kuendeleza ajenda ya Baraza,” akasema.
Nafasi hiyo ilibaki wazi baada ya Gavana Kahiga kujiuzulu Oktoba 22 kufuatia ukosoaji mkali wa umma kutokana na matamshi yake tata kuhusu kifo cha aliyekuwa waziri mkuu, Raila Odinga. Kauli yake, ambayo ilionekana na wengi kama kusherehekea kifo cha Bw Odinga, iliibua hasira kote nchini na wito wa kuondolewa kwake.
Dakika chache baada ya kutangaza kujiuzulu, Baraza la Magavana liliitisha kikao maalumu na kuamua kwa kauli moja kumwondoa rasmi katika wadhifa huo. Baadaye Kahiga aliomba msamaha, akisema matamshi yake yalikuwa ya kibinafsi na hayakupaswa kuhusishwa na Baraza.
Bw Odinga aliaga dunia Oktoba 15 alipokuwa akipokea matibabu nchini India. Alipewa mazishi ya kitaifa Oktoba 19, yaliyoongozwa na Rais William Ruto na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na wageni mashuhuri. Aliombolezwa sana kote nchini na viongozi wa kisiasa, mashirika ya kiraia na Wakenya wa kawaida.
Uchaguzi wa Gavana Njuki unajiri wakati Baraza linashughulikia masuala muhimu ya kitaifa kama ugatuzi, ushirikiano wa serikali za kaunti na ufadhili wa maendeleo.
Magavana wenzake walionyesha imani kuwa ataongoza kwa uthabiti na kuchangia pakubwa katika kazi za Baraza.
“Huu ni wajibu muhimu unaohitaji ushirikiano, haki na kujitolea. Tunaamini Gavana Njuki ataendeleza misingi ya Baraza na kuimarisha juhudi zetu katika kuendeleza utawala wa kaunti,” akasema Gavana Abdullahi.