Gavana Wanga atetea utawala wake ‘kanjo’ wakihusishwa na fujo za mikutano ya kisiasa
SERIKALI ya Kaunti ya Homa Bay imewatetea maafisa wake wanaotuhumiwa kuvuruga mikutano mbalimbali ikiwemo ya kisiasa.
Visa vya fujo vimeripotiwa siku za hivi karibuni Homa Bay na sasa maafisa wa ‘kanjo’ wamewekwa kwenye mizani kwa madai ya kutumiwa vibaya.
Tukio la majuzi zaidi ni la mnamo Februari 8 katika hafla ya kuchangisha pesa eneo la Kanyadato, Ndhiwa iliyohudhuriwa na Waziri wa Fedha John Mbadi na Katibu wa Wizara ya Usalama Raymond Omollo.
Baadhi ya washukiwa waliodaiwa kutibua mkutano, walikamatwa na kufikishwa mahakamani Ndhiwa. Kulingana na Mwenyekiti wa Shirika la Ustawishaji wa eneo la Kusini mwa Ziwa, Odoyo Owidi, ‘kanjo’ wanahusika na mashambulio yanayoshuhudiwa.
“Tuna picha na video za kuthibitisha haya,” akasema katika hafla ya mazishi mnamo Ijumaa iliyopita.
“Huwezi kuajiri watu kwa lengo la kusababisha vurugu katika kaunti. Maafisa hao wanafaa kusimamishwa kazi na kupigwa msasa tena kwa sababu huenda wakakosa kupita mtihani wa maadili,” akaongeza.
Dkt Omollo, ambaye alihudhuria mazishi hayo, aliahidi kuwa serikali itakabili matendo ya kiuhalifu.
“Tumekuwa na visa kadhaa vya wizi na fujo yakiwemo matukio ambapo watu waliaga dunia,” katibu akaeleza.
Hata hivyo, usimamizi wa kaunti umejitetea ukisema malalamishi yanayotolewa dhidi ya kaunti hayana mashiko.
Kwa mujibu wa Afisa Mkuu wa Mawasiliano katika Kaunti, Atieno Otieno, maafisa wa kaunti hufanya kazi kwa utaalamu na uwazi.
“Yeyote mwenye ushahidi kuhusu mtu ama idara ya kaunti yenye utovu wa maadili, awasilishe katika mamlaka husika kwa uchunguzi,” akaarifu kupitia taarifa mnamo Jumapili.
Bi Otieno alikemea visa vya fujo akiahidi kuwa gatuzi hilo liko tayari kushirikiana na vyombo vya usalama kuhakikisha sheria zinafuatwa.
“Tunaomba washikadau wote, wakiwemo wanaharakati wa kisiasa, wawe makini na wasitoe madai ambayo hayajathibitishwa ili wasitibue hali ya amani kwa kuibua taharuki,” akarai.
Vilevile, Serikali ya Kaunti ya Homa Bay ilitisha kuchukua hatua za kisheria kwa wanaotuhumu maafisa wake bila ushahidi wowote.