KATIKA kipindi cha takribani mwaka mmoja ujao, Sarah Nyambura, mwanafunzi wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 24, ataingia katika soko la ajira ambalo tayari limefurika.

Hata hivyo, tayari ana wasiwasi kwamba kampuni nyingi zinazidi kutegemea Akili Unde (AI), roboti za mawasiliano na mifumo ya kidijitali.

Kwa sasa, AI tayari imebadilisha jinsi mwanafunzi huyo wa mwaka wa nne wa uandishi wa habari anavyopanga mustakabali wa taaluma yake. Anafahamu fika kuwa baadhi ya ajira zitapitwa na wakati, na hata taaluma yake haijaepuka mabadiliko hayo. Hapatii kipaumbele ajira ya saa za kawaida za asubuhi hadi jioni na anaamini kuwa “awe na wasiwasi au la, AI iko hapa na haiondoki.”

Utafiti mpya umeonyesha kuwa wafanyakazi wanne kati ya watano wanaamini kuwa AI itaathiri majukumu yao ya kila siku kazini, huku kizazi cha Gen Z kikiwa miongoni mwa wanaoonyesha wasiwasi mkubwa zaidi kampuni zinapozidi kutegemea roboti za mazungumzo na mifumo ya kisasa.

Ripoti hiyo ya kimataifa ilitolewa na Randstad, mojawapo ya mashirika makubwa zaidi ya ajira duniani. Utafiti huo uliwahusisha wafanyakazi 27,000 na waajiri 1,225, na kuchambua zaidi ya nafasi milioni tatu za ajira katika sekta 35.

“Kizazi cha Gen Z ndicho chenye wasiwasi mkubwa zaidi, huku kizazi cha Baby Boomers kikionyesha kujiamini zaidi na kuwa na hofu ndogo kuhusu athari za AI na uwezo wao wa kuendana nayo,” ripoti hiyo ilisema.

Kwa kuzingatia kuwa Gen Z imekulia katika enzi ya mabadiliko ya haraka ya kiteknolojia, wengi wangetarajia kizazi hicho kuwa na mtazamo chanya kuhusu teknolojia mpya. Hata hivyo, si wote wanaokubaliana na hilo.

Adoyo Immaculate, mwenye umri wa miaka 23, anaelewa wasiwasi huo lakini anauona kwa mtazamo tofauti. Kwa maoni yake, hofu hiyo inatokana na kutojua na kukosa uelewa wa kutosha.

“Vijana wengi wana hofu kwa sababu hawajaonyeshwa jinsi AI inavyoweza kufanya kazi pamoja nao badala ya kupambana nao. Unapoelewa mipaka na uwezo wake, haionekani ya kutisha bali ni nyenzo tu,” anasema Bi Adoyo.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa karibu nusu ya wafanyakazi wa ofisini (asilimia 47) wanaamini kuwa AI itanufaisha kampuni zaidi kuliko wafanyakazi. Aidha, nafasi za ajira zinazohitaji ujuzi wa AI zimeongezeka kwa asilimia 1,587, ishara kwamba AI inachukua nafasi ya kazi rahisi na za kitaratibu.

Brian Khavalaji, mwenye umri wa miaka 27, anaamini kuwa AI, kama teknolojia nyinginezo, tayari imeanza kuvuruga namna kazi zinavyotekelezwa. Hata hivyo, anasema wale watakaoikumbatia mapema na kuitumia kwa njia inayofaa wana nafasi nzuri zaidi kupata ajira.

“AI ni kichocheo tu, ni chombo kinachowasaidia binadamu kuwa na ufanisi zaidi kazini,” anasema. Hata hivyo, anaonya kuwa kuitegemea kupita kiasi kunaweza kusababisha uzembe na kushuka kwa ubora wa kazi.

Mkurugenzi wa wafanyakazi wa Benki ya Diamond Trust na mwanzilishi wa Lillian Ngala Network, Bi Lillian Ngala, anasema hakuna njia ya kuepuka AI.

“Huwezi kumudu kutokumbatia AI. Haibadilishi kazi za watu, bali inakamilisha ujuzi uliopo ili tuwe na uzalizaji zaidi,” anasema, akihimiza vijana wa Gen Z kujifunza ujuzi unaohusiana na AI badala ya kuogopa.

Ripoti hiyo pia inaonyesha tofauti ya mtazamo kati ya waajiri na wafanyakazi kuhusu mustakabali wa biashara. Takriban asilimia 95 ya waajiri wanatarajia ukuaji mwaka huu, ilhali ni asilimia 51 pekee ya wafanyakazi walio na matumaini hayo.