Habari

Gharama ya kampeni za Raila AUC ni siri, Mwanasheria Mkuu aambia mahakama

Na SAM KIPLAGAT July 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MWANASHERIA Mkuu Dorcas Oduor amesema kuwa taarifa kuhusu kiasi cha fedha kilichotumiwa na serikali ya Kenya katika kampeni ya Raila Odinga kuwania Uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) ni siri ya serikali na inalindwa kisheria.

Katika pingamizi lililowasilishwa katika Mahakama Kuu, Bi Oduor pia anataka ombi la wakili Lempaa Suyianka, litupiliwe mbali kwa madai kuwa hakufuata utaratibu unaostahili wa kupata taarifa hiyo.

Anadai kuwa Bw Suyianka alipaswa kwanza kuwasiliana na Ofisi ya Malalamishi ya Umma (CAJ) kabla ya kuelekea mahakamani.

Kupitia Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, S.O. Kumba, serikali imesema kuwa taarifa ambayo wakili huyo anaomba inalindwa na Kifungu cha 6 cha Sheria ya Upatikanaji wa Habari, kwani inahusu masuala ya uhusiano wa kimataifa, usalama wa taifa na maamuzi ya Baraza la Mawaziri.

Hata hivyo, Bw Suyianka amesema aliandikia Wizara ya Masuala ya Kigeni Septemba 9 2024 lakini hakupokea jibu, na baadaye akaeleza CAJ kuwa hakupata taarifa aliyoomba.

Anadai kuwa kampeni ya Bw Odinga ilifadhiliwa kwa njia ya siri kwa kutumia fedha za umma ambazo hazikuidhinishwa na Bunge.

“Ni dhahiri kuwa serikali inataka kuficha matumizi ya fedha ya kampeni iliyoendeshwa kwa siri na watu wasiojulikana. Raia wana haki ya kujua jinsi fedha zao zilivyotumika,” alisema Bw Suyianka.

Wakili huyo anaitaka mahakama kuamua kuwa matumizi hayo yalikiuka Katiba, hususan Kifungu cha 201 kinachohusu uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma.

Mahakama sasa inasubiriwa kuamua ikiwa ombi hilo litasikilizwa au kutupiliwa mbali kama serikali inavyotaka.