Habari

Gideon Moi aacha wafuasi kwa mataa, ajiondoa uchaguzi Baringo baada ya kukutana na Ruto

Na FLORAH KOECH, FATUMA BARIKI October 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MWENYEKITI wa chama cha Kanu Gideon Moi amejiondoa kwenye kinyang’anyiro cha useneta Baringo, Taifa Leo sasa inaweza kuthibitisha.

Awali mjini Kabarnet Alhamisi Oktoba 9, 2025, wafuasi wake walifanya maandamano makubwa baada ya Bw Moi kukosa kufika kuidhinishwa na Tume ya Uchaguzi na Mipaka IEBC.

Kulingana na ratiba, Gideon alikuwa anatarajiwa kuwasili saa tano asubuhi, ila kufikia alasiri hakuwa ameonekana, jambo lililosababisha vurugu miongoni mwa wafuasi wake.

Jumatano, duru zilikuwa zimeambia Taifa Leo kwamba Gideon alikutana na Rais William Ruto kwenye mkutano wa faragha Ikulu. Duru zilisema kwamba mwenyekiti huyo wa Kanu alishawishiwa kujiondoa kwenye kura hiyo ili kumpa nafasi mwaniaji wa UDA kushinda.

Alhamisi ilikuwa siku ya mwisho ya kuwasilisha makaratasi ya uteuzi wa chama kwa ajili ya kuidhinishwa na IEBC.

Mwaniaji wa UDA Vincent Chemitei alifikisha makaratasi yake na kupewa idhini ya kushiriki kura.

Katibu Mkuu wa Kanu George Wainaina amethibitisha kwamba chama hicho hakitasimamisha mtu yeyote kwenye kura hiyo inayotarajiwa kufanyika Novemba 27.