Habari

Gideon Moi azua msisimko kwa kutangaza atawania kiti cha Baringo

Na CHARLES WASONGA October 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

BAADA ya kuwaweka wafuasi wake katika hali ya ngoja ngoja kwa muda mrefu, hatimaye mwenyekiti wa chama cha Kanu Gideon Moi amejitosa rasmi kwenye kinyang’anyiro cha useneta wa Baringo Novemba 27, 2025.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Alhamisi, Oktoba 2, 2025, mkurugenzi wa mawasiliano wa chama hicho Manase Nyaida alisema hatua hiyo imefikiwa kufuatia mashauriano ya kina na mwafaka kati ya wanachama wa Kanu na wakazi wa kaunti ya Baringo.

“Uamuzi wa kumteua Mheshimiwa Gideon Moi kuwa mwaniaji wa Kanu katika uchaguzi mdogo ujao wa useneta wa Baringo ni kielelezo cha kujitolea kwa chama kutoa uongozi wenye maono kwa wakazi wa Baringo na taifa kwa ujumla,” akaeleza.

Bw Nyaida alisema Moi amekubali uteuzi huo na kushukuru Kanu, wanachama na watu wa Baringo na uvumilivu wao na imani kwa sifa zake za uongozi.

“Ameahidi kuendesha kampeni itayoangazia sera zitakazofanikisha utekelezaji wa matakwa ya wananchi wa Baringo,” akaongeza.

Bw Moi sasa atapambana na mgombeaji wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) Vincent Kiprono Chemitei aliyeibuka mshindi katika mchujo wa chama hicho mwezi jana.

Bw Chemitei, 32, aliibuka kidedea kwa kuzoa jumla ya kura 48,791 katika kinyang’anyiro kilichoshirikisha wagombeaji wengine wanane.

Kiti hicho kilisalia wazi kufuatia kifo cha Seneta William Cheptumo wa UDA aliyembwaga Gideon katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2022.

Inabashiriwa kuwa kujitosa kwa Gideon katika kinyang’anyiro hicho kutafufua uhasama wa kisiasa kati yake na Rais William Ruto, ambaye anahusudiwa na wakazi wengi wa Baringo.

Ni kutokana na umaarufu wa Dkt Ruto na chama cha UDA katika kaunti hiyo ambapo, marehemu Cheptumo alimshinda Gideon katika uchaguzi mkuu wa 2022, kwa kupata kuwa 141, 177 dhidi ya 71,480 zake mtoto huyo wa rais wa zamani Daniel Moi.