GIKOMBA. Ndimi za moto zarudi kulamba mali ya mamilioni
Na PETER MBURU
BAADHI ya wafanyabiashara katika soko la Gikomba, Jijini Nairobi wanakadiria hasara tele baada ya moto mkubwa uliozuka katika sehemu ya soko hilo usiku wa kuamkia Jumatano kuchoma maduka na vibanda, ukiwaacha na hasara isiyojulikana.
Moto huo ambao uliripotiwa kuanza mwendo wa saa nane usiku uliteketeza sehemu iliyo na zaidi ya maduka na vibanda 100, pamoja na benki moja, ukichoma hadi saa tatu asubuhi wakati timu za uokoaji na wazima moto walifanikiwa kuuzima.
Timu za polisi wa kawaida, GSU, wazima moto na shirika la Msalaba mwekundu zilishirikiana kuuzima moto huo, huku mamia ya wafanyabiashara na wakazi wa karibu na soko hilo wakifurika kujitazamia hasara uliosababisha moto huo.
Wafanyabiashara waliozungumza na Taifa Leo walisema kuwa moto huo uliwasababishia hasara ya maelfu, huku wengine wakiwa bado walikuwa wamezuiliwa kufika eneo yalipokuwa maduka yao na polisi kutokana na moto.
“Hapa tumeenda hasara ya Sh700,000 ya bidhaa pamoja na ujenzi. Tunaomba serikali iharakishe mpango ambao ilituahidi wa kutujengea soko namna inavyofaa ili tuepuke hasara kama hizi. Hapa ndio tunategemea,” akasema Bw Jeremiah Galgalo, ambaye duka lake la viatu liliteketea lote.
“Kila wakati kunapotokea moto ni sisi tunaumia tu kwani huwa tunajijengea. Sasa hatuna kitu cha kufanya,” akasema.
Bi Joan Njeri naye pamoja na mamia ya watu wengine walikuwa wamezuiliwa eneo mbali na ulipokuwa moto, akisema hakujua kiwango cha hasara ambacho biashara yake ya nguo iliadhirika.
Vilevile, wakazi wa karibu na soko hilo walipongeza timu za uokoaji kwa kufika haraka, wakisema hatua hiyo ilisaidia moto kutoenea sehemu kubwa.
“Wakati huu wazima moto walifika kwa haraka na kufanya bidii wakishirikiana na baadhi ya wakazi kuuzuia moto huu kuenea katika sehemu kubwa. Tunashukuru sana. Lakini tunaomba serikali inapoangalia suala hili iangazie sote wakazi wa hapa na wafanyabiashara pia kwani wakazi huwa tunasahaulika,” akasema Bi Eunice Ngendo, mkazi.
Bi Ngendo alisema kuwa baadhi ya vibanda katika soko hilo vimejengwa karibu sana na nyumba za wakazi na hivyo kila kunapotokea visa vya moto, huwa wanaadhirika kwa kuchomekewa na moshi mkubwa unaotoka.
Kwa bahati nzuri, hakukuwa na kisa cha majeruhi wala vifo kilichoripotiwa katika mkasa huo, kama namna imekuwa katika mikasa ya mbeleni.
Shirika la Msalaba Mwekundu kupitia akaunti yake ya Twitter lilisema litakadiria kiwango cha hasara iliyotokana na moto huo, matamshi ambayo yalirejelewa na serikali.
“Hakuna visa vya majeruhi vilivyoripotiwa. Kenya Redcross itafanya ukaguzi,” likasema shirika hilo.
“Moto umezimwa na tuko katika shughuli za kufanya ukaguzi wa hasara. Tunawarai wafanyabiashara kutuwia radhi wakati tunapoendelea kulifanya eneo hili salama kwao kurejea tena,” akasema Bw Moses Lilan, naibu kamishna wa kaunti Jijini Nairobi.
Mnamo Juni mwaka huu, watu 15 walifariki na wengine 60 kujeruhiwa vibaya baada ya moto mwingine kuzuka katika sehemu ya soko hilo.
Mwaka uliopita, baadhi ya wafanyabiashara wa Gikomba walipokea hasara ya Sh15milioni wakati moto mwingine ulizuka.
Ni majuzi tu ambapo Rais Uhuru Kenyatta alikataa kusoma hotuba yake katika kongamano na wafanyabiashara wadogo, akisema alijutia kuwa bado hajatimiza ahadi yake kwa wafanyabiashara wadogo haswa wa soko la Gikomba kuwaboreshea soko.
Soko hilo lina takriban watu 14, 000 ambao hufanya biashara.