Habari

Githu ataka cheo cha Waziri Mkuu, naibu kibuniwe

October 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Mwanasheria Mkuu Githu Muigai sasa anaunga mkono mageuzi ya Katiba yatakayopanua kitengo cha utawala kwa kubuni nyadhifa kama vile Waziri Mkuu na manaibu wake wawili ambao pia watahudumu kama wabunge.

Amesema washikilizi wa nyadhifa hizo wanapaswa kuwajibika moja kwa moja kwa bunge badala ya hali ilivyo kwa sasa ambapo ushirikiano kati ya bunge na serikali kuu ni mdhaifu kwa sababu mawaziri si wabunge.

“Tunahitaji mfumo wa ubunge ambapo kiongozi wa serikali ambaye ni waziri mkuu ambaye atakuwa mbunge na hivyo kuwa na nafasi ya kutangamana na wabunge kila mara kushughulikia masuala ibuka haraka. Mfumo wa sasa wa urais uonekana kuchelewesha kazi ya bunge,” amesema Profesa Muigai.

Amesema hayo Jumanne alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Utekelezaji wa Katiba (CIOC) katika majengo ya bunge ili kutoa maoni yake kuhusu suala la iwapo katiba ya sasa inapaswa kufanyiwa mageuzi au la. Kamati hiyo inaongozwa na Mbunge wa Ndaragua Jeremiah Kioni.

“Serikali inapaswa kupanuliwa kama ilivyo katika taifa la Japan ili kuimarisha uwajibikaji katika utendakazi wa serikali kwa manufaa ya wananchi,” Bw Muigai akasema.

Msomi huyo ambaye sasa amerejelea kazi ya uwakili pia amependekeza kuwa baadhi ya mawaziri wawe wakiteuliwa kutoka miongoni mwa wabunge “ili kuimarisha uhusiano wa karibu kati ya serikali kuu na bunge.”

Machafuko

Wazo la Profesa Muigai linaonekana kushabihiana na lile la kiongozi wa ODM Raila Odinga na baadhi ya viongozi wa makanisa ambao wamedai kuwa mfumo wa sasa wa urais ndio huchangia kutokea kwa machafuko ya kisiasa kila baada uchaguzi mkuu.

Kuhusu upinzani, Profesa Muigai alipendekeza kubuniwe kwa afisi ya kiongozi rasmi wa upinzani ambayo itafadhiliwa na mfuko wa umma kuhakikisha “kuwa upinzani unaikosoa serikali”.

“Utendakazi wa serikali hauhakikiwi ipasavyo wakati huu kwani baada ya muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, inaonekana kuwa upinzani umegeuka butu hasa bungeni. Inasikitisha kuwa wabunge ambao wanapaswa kuihakiki serikali ndio wamegeuka kuwa wafuasi wake sugu,” akasema.

Kulingana na Profesa Muigai suala la kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia linaweza tu kusuluhishwa ikiwa sheria ya uchaguzi itageuzwa ili wabunge wawili, mwanamume na mwanamke, wawe wakichaguliwa katika kila eneobunge.

Hii ina maana kuwa ikiwa wazo hili litakubalika, bunge la kitaifa litakuwa na jumla ya wabunge 580, wawili kutoka maeneobunge 290 ya sasa.

Miongoni mwa wanasheria waliofikia mbele ya kamati hiyo ili kutoa maoni yao kuhusu marekebisho ya Katiba, ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Profesa Yash Pal Ghai na aliyekuwa mshauri wa Rais kuhusu masuala ya Katiba Abdikadir Mohamed.

Shinikizo za marekebisho ya Katiba ya sasa zinaendeshwa kupitia mswada wa Punguza Mizigo chini ya kiongozi wa chama cha Thirdways Alliance Ekuru Aukot na Jopokazi la Maridhiano (BBI) lililoteuliwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga.