Habari

Giza madaktari wakigoma

December 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

WAKENYA wanakumbwa na hali ya mahangaiko pamoja na hofu ya kukosa huduma za matibabu baada ya madaktari katika hospitali za umma kutangaza kuanza mgomo wa kitaifa leo Jumatatu kutokana na kile walichotaja kuwa kusambaratika kwa mazungumzo kati yao na ya serikali.

Sekta ya afya sasa inagubikwa na giza huku wagonjwa wakiteseka mno msimu huu wa janga la corona.

Viongozi wa chama cha kutetea maslahi ya madaktari na wataalamu wa meno (KMPDU), walitangaza kuwa, mazungumzo yao na serikali yaliyochukua miezi minane hayakuzaa matunda.

Mgomo huo utakuwa wa tatu wa wahudumu wa afya kwa kuwa wauguzi na maafisa wa utabibu wanaendelea na mgomo wao ambao umelemaza huduma katika hospitali za umma.

Tangu wahudumu hao wagome siku 14 zilizopita, wagonjwa maskini wamekuwa wakihangaika kupata huduma za matibabu katika hospitali na vituo vya afya vya umma.

Hali sasa inatarajiwa kuwa mbaya zaidi kufuatia mgomo wa madaktari ambao waliuahirisha wiki mbili zilizopita kutoa nafasi kwa mazungumzo.

“Tunataka kufahamisha umma kwamba, tutasusia kazi kulingana na katiba ya Kenya kwa sababu ya masuala ambayo hayajatatuliwa,” alisema Kaimu Katibu mkuu wa KMPDU, Dkt Chibanzi Mwachonda.

Ingawa wabunge walikuwa wamejitolea kupatanisha madaktari na serikali, juhudi hizo ziligonga mwamba huku Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe akiagiza wahudumu wanaogoma wafutwe kazi.

“Wale ambao wako nje ambao wanataka kazi na wanataka kuendelea na kazi, wakati huu ndio sasa walete barua zao waajiriwe kazi na hiyo maneno iishie hapo,” Bw Kagwe alisema Jumamosi alipohudhuria mazishi ya aliyekuwa waziri Joe Nyagah katika Kaunti ya Embu.

“Lakini sana sana, tungependa kuendelea na wale ambao tuko nao tusikizane vizuri tuendelee na kazi. Hiyo ndio ile Krismasi ingekuwa nzuri. Hatutaki mtu kusema mwaka uliopita alikuwa na kazi na mwaka ujao unajiunga na wasio na kazi,” Bw Kagwe alisema.

Ingawa Bw Kagwe anatisha kuwafuta kazi wahudumu wa afya wanaogoma, hakuna hakikisho kuwa watakaoajiriwa hawatagoma wakilalamikia masuala sawa na watakaofutwa.

Waziri alisema wahudumu hao wanafaa kurejea kazini mazungumzo kuhusu malalamishi yao yakiendelea hasa msimu huu wa sherehe za Krisimasi.

Kulingana na Bw Kagwe, mambo mengi hutendeka msimu huu wa krisimasi yanayohitaji huduma za afya na migomo inayoendelea inaweza kusababisha maafa makubwa.

Kufuatia misimamo mikali ya wahudumu wa afya na serikali, Wakenya wanakodolea macho balaa kubwa msimu huu wa janga la corona baada ya madaktari kumpuuza.

Hatima ya wagonjwa zaidi ya 900 wa corona wanaolazwa katika hospitali za umma, hasa walio katika wadi za wagonjwa mahtuti imo hatarini.

Ni madaktari wanaoanza mgomo leo ambao wamekuwa wakiwashughulikia wagonjwa katika hospitali baada ya wauguzi na matabibu kugoma.

Mshirikishi wa mashirika ya kijamii Suba Churchill alisema mgomo wa madaktari utalemaza sekta ya afya nchini.

“Hlii litakuwa pigo kwa sekta ya afya wakati maambukizi ya corona na vifo vinazidi kuongezeka, wakazi wa mijini wakisafiri maeneo ya mashambani kwa sherehe za krisimasi” alisema.

Wahudumu wa afya wanasema matakwa yao yanaweza kuafikiwa na kulaumu serikali kwa kutokuwa na nia njema katika mazungumzo. Wanataka marupurupu ya kuhatarisha maisha yao hasa wakati huu wa janga la corona na vifaa bora vya kujikinga, bima ya afya na kupandishwa vyeo.

Ikiwa serikali haitachukua hatua za kusitisha mgomo huo, utakuwa mkubwa zaidi kufanywa na wahudumu wa afya.

Wanafamasia, wataalamu wa maradhi tofauti, wakuu wa hospitali wanatarajiwa kujiunga na mgomo huo.

“Tumelegeza msimamo na kuvumilia sana. Chama kilisimamisha mgomo kutoa nafasi ya mazungumzo lakini hayajazaa matunda, mgomo utaanza Jumatatu  (leo),” Bw Mwachonda alisema.