Habari za Kaunti

Afidiwa Sh6.9 milioni kwa kutolewa katika kundi la WhatsApp kazini na kufutwa

Na JOSEPH WANGUI September 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA waziri katika Kaunti ya Tharaka-Nithi, ambaye matatizo yake yalijumuisha kutengwa na kufungiwa nje ya kundi jipya rasmi la WhatsApp ambalo wenzake walikuwa wakiwasiliana, amefidiwa Sh6.9 milioni na Mahakama kwa kufutwa kazi kinyume cha sheria.

Bi Beatrice Kathomi Kinyua, alipatiwa fidia hiyo na Mahakama ya Mahusiano ya Kazi na Ajira baada ya kupata kwamba alifutwa kazi  kinyume cha sheria.

Mahakama ilibaini kuwa kutimuliwa kwake kazini Januari 2025 kulikuwa kinyume na haki zake za kikatiba, ikiwemo haki ya kutotengwa na kufuatwa kwa taratibu za haki katika ajira.

Jaji Onesmus Makau alisema, “Kwa kuzingatia jinsi alivyofukuzwa bila kuzingatia haki zake za kikatiba, na ukweli kwamba alitarajia kuendelea na kazi kwa miaka mitatu zaidi, na pia kuwa hana nafasi ya kupata kazi yenye mshahara sawa ndani ya mwaka mmoja, nampa fidia ya mshahara wa miezi 12.”

Bi Kinyua alifukuzwa baada ya zaidi ya miaka miwili akiwa katika nafasi hiyo, huku serikali ya kaunti ikimshutumu kwa kushindwa kujibu barua za maelezo na kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Hata hivyo, mahakama iligundua kuwa hakuna ushahidi wa kutosha kuunga mkono madai hayo.

Aidha, alidai alitengwa katika mawasiliano rasmi ya viongozi wa kaunti, ikiwemo kufukuzwa kwenye kikundi kipya cha WhatsApp cha CEC, jambo lililochukuliwa kama njia ya kumwonea na kumchochea kujiuzulu.

Serikali ya kaunti ilikana madai hayo na kusema kuwa upungufu wa magari rasmi ndio sababu ya kugawanywa kwa magari kwa viongozi wa CEC, lakini jaji Makau alisema kuwa kupewa gari baadhi ya viongozi huku wengine wakizuiliwa ni ubaguzi.

Mahakama pia ilikumbusha kuwa mchakato wa kufukuzwa ulikiuka haki ya Bi Kinyua ya kupata usikilizwaji wa haki kabla ya kufutwa kazi, jambo linalotakiwa na sheria.

Bi Kinyua alipata fidia ya Sh4.9 milioni kwa kufukuzwa kinyume cha sheria na Sh2 milioni kwa uharibifu wa heshima na haki zake za kikatiba, lakini mahakama ilikataa ombi lake la kurejeshwa kazini kutokana na kuvunjika kwa uhusiano kati yake na serikali ya kaunti.