Afueni eneo likipata hospitali ya kwanza miaka 60 baada ya uhuru
WAKAZI wa kijiji kimoja katika Kaunti ya Kajiado wamepata afueni baada ya kituo kipya cha afya kujengwa na kuwapunguzia mateso ya miaka mingi wakitafuta huduma za kimsingi za afya.
Wakazi wa Oloilalei katika Wadi ya Entonet Lenkisim katika Kaunti Ndogo ya Kajiado Kusini hawatalazimika tena kusafiri kwa zaidi ya kilomita 30 kupata huduma za kimsingi za afya.
Wakazi hao walilazimika kusafiri hadi hospitali ya Mashuru Level Four, safari inayochukua siku nzima.
Lakini sasa wakazi hao watafurahia huduma za matibabu katika Hospitali Mpya ya Chief Mpaa ambayo awamu ya kwanza iliyogharimu Sh 200 milioni imefunguliwa kwa wananchi.
Hospitali ina sehemu ya wagonjwa wa kulazwa na wa kutibiwa na kurudi nyumbani, wodi ya kisasa la uzazi, maabara, na duka la dawa.
Wakati wa ufunguzi rasmi wa kituo hicho cha afya mnamo Ijumaa, wakazi walifurahi wakati Gavana Joseph Ole Lenku alipowasili na wahudumu wapya kuanza kazi.
Wenyeji wa eneo hilo, hasa wanawake, walisema kituo hicho ni ndoto baada ya miaka mingi ya kutembea mbali kutafuta huduma za afya.
“Tumeteseka kwa miaka mingi. Tulilazimika kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za msingi za matibabu. Baadhi ya wanawake wajawazito wamejifungua kando ya barabara nyakati za usiku wakielekea hospitali,” alisema Eunice Sakimba, mkazi.
Gavana wa Kajiado Joseph Ole Lenku alisisitiza kujitolea kwa utawala wake kuhakikisha angalau vijiji vyote vya mashambani vina kituo cha afya kinachofikika kwa urahisi.
“Licha ya tatizo la rasilimali, tunajitahidi kuimarisha huduma za afya kwa wote hasa katika maeneo ya mashambani. Vituo hivyo pia vinahitaji maji na nishati. Kaunti imechagua nishati endelevu ya kijani katika vituo vyote vya umma,” Gavana Lenku alisema.
Kituo hicho pia kitatoa mafunzo kwa wanafunzi wa ndani katika kozi mbalimbali ili kuongeza upatikanaji wa wataalam wa matibabu sio tu hospitalini bali pia katika Kaunti.