Ahadi ya Ruto kugawia Taita-Taveta mapato ya mbuga ya Tsavo yafifia
SERIKALI imeashiria kubadilisha mawazo yake ya kuipa Kaunti ya Taita Taveta mgao wa asilimia 50 ya mapato kutoka kwa mbuga ya Tsavo iliyokuwa imeahidiwa na Rais William Ruto.
Akiongea na wadau wa sekta ya utalii katika eneo la Mwatate, Waziri wa Utalii na Wanyamapori, Dkt Alfred Mutua, alisema sheria itapitishwa na bunge la kitaifa kusimamia ugavi ambao utategemea uwezo wa kifedha wa serikali ya kitaifa.
Mnamo Julai mwaka jana, Rais Ruto aliahidi wenyeji kuwa kutakuwa na mgao sawa, hata hivyo waziri Mutua alipendekeza njia tofauti ya ugavi wa mapato, huku akisisitiza umuhimu wa kuwepo wa sheria ili kuhalalisha makubaliano hayo.
Waziri Mutua aliwahakikishia wenyeji kuwa ahadi hiyo ya Rais itatimizwa hivi karibuni.
“Haitakuwa 50-50 lakini kutakuwa na kugawanywa kwa namna fulani. Lazima kuwe na sheria na tayari inaandaliwa,” alisema akijibu ombi la Gavana Andrew Mwadime la kuharakisha mchakato huo.
Akihutubia waandishi wa habari, Bw Mutua alisema kuna sheria inayoandaliwa itashughulikia swala la ugavi wa mapato hayo.
“Tunaunda mswada ambao tutauwasilisha bungeni kisha tutakubaliana kuhusu ugavi kulingana na mapato na kuwepo kwa rasilimali na fedha za kuwezesha mipango ya serikali,” alisema.
Bw Mutua alisema wizara itafanya zoezi la kushirikisha umma ndani ya miezi mitatu ili kupata maoni kutoka kwa wakazi kwa ajili ya kuundwa kwa mswada huo.
Tangu Rais athibitishe ahadi yake, viongozi wa kaunti hiyo wamekuwa wakisukuma idara husika kuhakikisha ahadi hiyo inatekelezwa.
Gavana Mwadime alisema ahadi hiyo ililenga kuleta usawa katika ugavi wa rasilimali nchini.
Mbuga ya Tsavo, inamiliki asilimia 62 ya ardhi ya kaunti hiyo ilihali mapato yanayotokana na hifadhi hiyo hayajawahi kufaidisha eneo hilo.
Gavana Mwadime aliomba serikali ya kitaifa kuharakisha mchakato huo ili kuwaruhusu wakazi hao kufaidika na wakati huo huo kuongeza mapato ya kaunti.
“Tulitaka kupewa mbuga tuisimamie lakini hiyo inaonekana kuwa haiwezekani kwa sasa. Tumekubali tuanze kupata mgao kidogo tukiendelea kupigania mbuga hii igatuliwe,” alisema.
Mwaka jana, baadhi ya wawakilishi wa bunge la kaunti waliwasilisha maombi yao kwa bunge la kitaifa, wakiwataka wabunge kuingilia kati na kuhakikisha kuwa kaunti ya Taita Taveta inapata mgao wa mapato ya Tsavo.
“Tunataka kufurahia manufaa ya mbuga hii iliyoko katika kaunti yetu. Naomba wizara ifuatilie ombi hilo ili tuweze kusuluhisha masuala yetu,” alisema mwakilishi wa Mwatate Bw Keneddy Mwalegha.
Baadhi ya viongozi wa kaunti hiyo pia wamekuwa wakijadili iwapo mbuga hiyo inafaa kubadilishwa kuwa hifadhi, huku usimamizi ukikabidhiwa serikali ya kaunti.
Katika mahojiano ya hivi majuzi, seneta Jones Mwaruma alisema hatua hiyo itaipa kaunti ya Taita Taveta udhibiti kamili wa mbuga hiyo na itaongeza mapato yake.
“Ikiwa Rais alikabidhi kaunti ya Kajiado hifadhi ya Amboseli kwa nini sisi pia hatupewi Tsavo?” alisema.
Hata hivyo, kaunti jirani zikiwemo Kitui, Makueni, Kilifi, Kwale, Tana River, na Kajiado pia huenda zikadai mgao wao kwani pia zinapakana na Tsavo.