Habari za Kaunti

Ajabu kaunti ya Narok ikitumia Sh8 milioni kuweka alama kwa masikio ya vifaru 20

Na MOSES NYAMORI March 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAUNTI ya Narok ilishindwa kueleza jinsi ilivyotumia Sh8 milioni kuweka alama kwenye masikio ya vifaru 20 weusi katika Hifadhi ya Kitaifa ya Maasai Mara.
Uongozi wa Gavana Patrick Ntutu pia haukuweza kueleza kiasi cha pesa kilichotumika kununua mafuta yaliyotumiwa wakati wa zoezi hilo.

Zaidi ya hayo, fomu za uwasilishaji, fomu za toleo la kaunta (S11) na fomu za stakabadhi za kaunta (S13) hazikutolewa ili kuthibitisha matumizi ya Sh901, 000 zaidi kwa ununuzi wa dawa, kulipa mawakala, kununua vifaa vya kuchezea na vifaa vya matibabu.

Afisa wa kaunti hiyo pia anamulikwa kwa matumizi ya Sh2, 172, 800 na Sh1, 568, 000 zilizolipwa kwa wafanyikazi wa Idara ya Utalii na Huduma ya Wanyamapori Kenya mtawalia, ambayo haikuwa kwenye Mkataba wa Maelewano na Idara na Huduma.

Zaidi ya hayo, kampuni iliyokodishwa kwa utoaji wa huduma za helikopta haikuwa katika orodha ya watoa huduma waliosajiliwa kwa Mtendaji wa Kaunti kwa mwaka unaoangaziwa.

“Katika hali hiyo, usahihi na ukamilifu wa kiasi cha matumizi cha Sh8, 141, 800 haukuweza kuthibitishwa,” inafichua ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu ya mwaka unaoishia Juni 30, 2014.

Katika Kaunti ya Kilifi, huenda Sh44 milioni zilizotumika katika ununuzi wa chakula cha msaada kwa wakimbizi katika kaunti hiyo zimepotea.

Kulingana na ripoti hiyo Sh44, 639, 728 zilitumika kulipia msaada wa dharura na usaidizi wa wakimbizi yaliyotolewa kwa kampuni nne kwa ajili ya usambazaji na utoaji wa chakula cha msaada.

Hata hivyo, haijulikani ikiwa vifaa husika vilifika kwa walengwa.

Katika mwaka unaoangaziwa, jumla ya Sh250, 000, 000 zilitumwa kwa hazina ya dharura, huku kaunti chini ya Gavana Gideon Mung’aro ikiashiria kuwa ilitumia duka kuu kupokea na kusambaza chakula kilichonunuliwa.

Hata hivyo, ripoti zilizothibitisha kiasi kilichopokelewa na kutolewa hazikutolewa.

Zaidi ya hayo, maelezo ya magari yaliyotumika kusambaza vifaa hivyo hayakutolewa.

Kaunti ya Tana River, pia inamulikwa kwa malipo yasiyo ya kawaida ya usafiri wa kigeni na marupurupu ya Sh6 milioni.

Kaunti hiyo ililipia gharama za usafiri kutoka nje ya nchi ya Sh26, 503, 679 ambapo Sh6, 395, 500 zilitumika kama wafanyakazi walipokuwa wakihudhuria Jumuiya Trade Investment and Education Exchange Mission nchini Amerika.

Kaunti hiyo pia inachunguzwa kuhusu uwezekano wa hasara ya Sh170, 895, 999 iliyotokana na gharama za bima.
Kiasi hicho kinajumuisha bima ya matibabu ya wafanyakazi ya Sh149, 999, 999 iliyolipwa mapema bila utaratibu.