Habari za Kaunti

Aliyemuua mwanamke kwa kumdunga kisu mara tano atupwa jela miaka 30

Na CHARLES WANYORO October 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA kuu ya Meru imemhukumu mlinzi mmoja kufungwa jela miaka 30 baada ya kumpata na hatia ya mauaji ya kikatili ya mwanaharakati wa haki za binadamu miaka miwili iliyopita.

Jaji Edward Muriithi aliamua kuwa Bw Patrick Naweet alinuia kumuua Bi Elizabeth Ekaru, alipomdunga kwa kisu mgongoni, shavuni, mapajani na kiganjani

Jaji alisema Bw Naweet alijua kwamba jinsi alivyomshambulia mwanaharakati huyo aliyekuwa na umri wa miaka 49, angemsababishia Bi Ekaru madhara makubwa au kumuua.

Alitupilia mbali maelezo ya mzee huyo wa miaka 50 kwamba alimdunga kisu marehemu ili kujilinda, akitaja asili ya majeraha, moja likiwa na kina cha sentimita 21.

Jaji Muriithi alisema kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha bila shaka kwamba Bw Naweet alipanga kumuua Bi Ekaru alipomshawishi kutoka kwa nyumba ya rafiki yake eneo la Kambi ya Garba katika mji wa Isiolo.

Mshtakiwa alimwendea marehemu mnamo Januari 3, 2022 na kumtaka amuonyeshe mpaka wa ploti yake, ambayo ilikuwa karibu na yake.

Hata hivyo, Jaji Muriithi alipuuzilia mbali utetezi huo, akisema kuwa licha ya Bw Naweet kutowasilisha ushahidi wa kushambuliwa, madai ya kupigwa kwa jiwe na kofi hayakuhalalisha kitendo hicho cha kinyama.

Jaji Muriithi alikubaliana na kiongozi wa mashtaka Eric Masila na wakili Zaina Kombo kwamba Bw Naweet alikuwa na nia ya kumuua Bi Ekaru.

Imetafsiriwa na Benson Matheka