Aliyenaswa akiwa na pingu akana kujifanya polisi
NA BRIAN OCHARO
MSHUKIWA wa uhalifu aliyekamatwa akiwa na pingu amekanusha mashtaka na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh600,000.
Bw Salim Muya Salim alishtakiwa Jumanne mbele ya mahakama ya Mombasa kwa makosa matatu ya kujifanya polisi na askari (kanjo) wa serikali ya Kaunti ya Mombasa.
Pia, alishtakiwa kwa kosa moja la kutoa taarifa za uongo kwa afisa wa umma.
Bw Salim pia alishtakiwa kwa kumiliki vitu vya serikali ambapo mahakama iliambiwa kuwa alipatikana na pingu mbili za polisi ambazo ni mali za Idara ya Polisi nchini.
Mahakama iliambiwa mshukiwa alipatikana na vitu hivyo licha ya kufahamu kuwa viliibwa au kupatikana kinyume cha sheria.
Pia, jamaa huyo alishtakiwa kwa kumuibia Bora Bevungwe Vungwe Sh9,000.
Mshtakiwa alidaiwa kutenda makosa yote kati ya Februari 23, 2024 na Septemba 4, 2023 katika eneo la Ganjoni, Kaunti Ndogo ya Mvita.
Alikana mashtaka yote alipofika mbele ya Hakimu Mkuu mkazi wa Mombasa, Bi Rita Orora.
Kiongozi wa mashtaka, Henrietta Mburu aliiomba mahakama kumwachilia mshukiwa kwa masharti magumu ya dhamana kutokana na mashtaka mengi yanayomkabili.
Hakimu huyo alimwachilia mshukiwa kwa dhamana ya Sh600,000 na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho.
Kwingineko, bidhaa mbalimbali zenye thamani ya zaidi ya Sh145 milioni zitaondolewa katika bandari ya Mombasa baada ya kampuni tano kushindwa kuzuia Mamlaka ya Bandari za Kenya (KPA) na Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA), kutoa mizigo hiyo iliyohifadhiwa kwenye makontena manne.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Mombasa, Kizito Magare, aliamua kwamba kampuni hizo tano zote zilikosa kuthibitisha kwamba zina maslahi kisheria kuhusiana na umiliki wa bidhaa hizo ili kusitisha mchakato wa kuziondoa kwenye bandari.
“Nakubaliana na maelezo ya washtakiwa kuwa ingawa walalamishi waliwasilisha stakabadhi za umiliki wa awali, hakuna ushahidi wowote uliotolewa kuonyesha kuwa wao ndio wamiliki wa sasa wa bidhaa hizo,” alisema jaji Magare.
Kwa mujibu wa mahakama, stakabadhi zote zilizowasilishwa mbele yake zinaonyesha kuwa bidhaa hizo zinamilikiwa na kampuni ya Dooba Enterprises Ltd.
Kampuni hizo tano ziliomba amri ya muda ya kuzuia Mupeki Hauliers Ltd, KRA na KPA, mawakala wao husika na au wasafirishaji kuondoa, kusafirisha na au vinginevyo kuondoa sehemu yoyote ya bidhaa mbalimbali kutoka bandarini.
Pia, walitaka uamuzi kwamba kampuni ya Dooba Enterprises Ltd haikuwa imepata haki ya kudai mali hizo kwa hivyo haiwezi kuchukuliwa kihalali au kuambatishwa na kampuni ya Mupeki Hauliers Ltd.
Kampuni hizo pia ziliomba amri ya kuachilia bidhaa zote kwao na nyingine ikitaka kampuni ya Mupeki Hauliers Ltd kulipa gharama za kesi hiyo, malipo ya bandarini kuanzia tarehe bidhaa hizo zilitangazwa kuchukuliwa kimakosa hadi malipo hayo yakamilike.
Hata hivyo, washtakiwa walidai kuwa wakuu wa kampuni hizo tano hawakuthibitisha kisheria kuwa wao ndio wamiliki wa bidhaa hizo.