Arati adai Waziri Machogu anahusika katika ghasia za majuzi Kisii
NA WYCLIFFE NYABERI
GAVANA wa Kisii Simba Arati amesema hatashiriki mazungumzo yoyote ya kumpatanisha na hasimu wake wa kisiasa, Sylvanus Osoro, mbunge wa Mugirango Kusini.
Kufuatia malumbano kati ya wawili hao, ambayo sasa yameanza kutishia maisha ya wakazi wa Kisii, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu aliwaandikia nyaraka viongozi hao akiwataka awapatanishe ili kuzika tofauti zao.
Lakini siku moja baada ya Machogu kuonyesha nia hiyo, Gavana Arati amesema hatashiriki mazungumzo yoyote hadi sheria ichukue mkondo wake kwa wapangaji wa ghasia hizo.
Akizungumza alipohudhuria hafla moja ya Kanisa Katoliki Jumamosi, Januari 13, 2024 katika eneobunge la Bomachoge Chache, Arati alimshutumu Machogu na kushangaza, akidai hata waziri huyo ana mkono katika kuhangaishwa kwake.
“Huwezi kusema sasa unataka kutupatanisha ilhali unajua kinachoendelea na unahusika katika fujo hizo kisiri. Machogu ni mtu niliyemshinda kura za ugavana vizuri lakini rais alimwonea huruma na kumteua serikalini. Licha ya hayo, hajakubali na wao ndio wanaopanga fujo dhidi yangu. Huwezi kuwa refa, kocha, mchezaji, mwamuzi, na msaidizi wake kwa wakati mmoja. Mimi sitashiriki mazungumzo yoyote hadi sheria ifuatwe,” Gavana Arati alidai.
Mnamo Ijumaa, Januari 12, 2024, Machogu aliwaandikia barua Arati na Osoro akiwaita vikao vya kutafuta suluhu ya purukushani zao za mara kwa mara.
Vikao hivyo vilipangwa kuanza Jumatano hii, Januari 17, 2024.
Kwenye barua yake, Machogu alitaja ghasia zinazoendelea Kisii kama ‘za kutatanisha na kusumbua’ na kuongeza kuwa zinadumaza ustawi na utulivu ambao jamii ya Abagusii imeishi nao kwa miaka mingi.
“Ili kupata undani wa suala hilo nimeamua kuwa mashauriano yaanzishwe kati ya viongozi ili kutafuta suluhu ya hali hii isiyokubalika inayotishia kuchafua jina zuri la eneo letu ambalo halina amani tena, ” ilisoma sehemu ya barua ya Machogu.
Kumsaidia kuwazungumzia mahasimu hao, Machogu ambaye ndiye kiongozi mwenye hadhi kuu serikalini kutoka jamii ya Abagusii, atawahusisha askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Kisii Joseph Mairura, Mhubiri Dkt Leonard Aencha wa dhehebu la Kiadventista (SDA) na Mhubiri Dkt Moses Mogita wa makanisa ya kiroho.
Mwanasheria Mkuu wa serikali Shadrach Mose pia alialikwa kwenye mashauriano hayo.
Miito ya kutaka Machogu na viongozi wa makanisa kuitisha mashauriano baina ya viongozi wa Kisii wanaozozana, imekuwa ikitolewa mara kwa mara na viongozi wengine akiwemo seneta Richard Onyonka.
Hata wazee wa Baraza la jamii ya Abagusii wamesema hawajawahi kushuhudia siasa chafu kama za sasa katika eneo hilo hata wakati wa zama za aliyekuwa kinara wa siasa zao marehemu Simeon Nyachae.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Abagusii Araka Matundura, ni mmoja wa washikadau ambao wametoa wito wa viongozi kushauriana na kuzika tofauti zao.
Bw Araka alionyesha kusikitishwa kwake na ghasia kama za Jumatatu wiki jana (Januari 8, 2024) ambapo kulikuwa na ufyatulianaji risasi katika eneobunge la Mugirango Kusini.
Ghasia hizo ziliwaacha watu wanne na majeraha mabaya ya risasi, huku magari mengi yakipasuliwa vioo.
Katika kisa kingine cha Juni 2023, katika Wadi ya Boikang’a Mugirango Kusini bado, Arati na Osoro walifarakana na kupelekea wafuasi wa viongozi hao kuanza kupigana kwa mishale na mikuki.
Mwaka 2021, katika mazishi ya babake aliyekuwa naibu gavana wa Kisii Joash Maangi, Osoro (UDA) na Arati (ODM) walilimana mangumi mbele ya vinara wao Rais William Ruto na Raila Odinga kujaribu kuwafurahisha.
Kufuatia purukushani za hivi punde za ufyatulianaji risasi, chama cha ODM kupitia Katibu Mkuu Edwin Sifuna kilielezea hofu zake kwamba maisha ya Gavana Simba Arati yalikuwa hatarini.
ODM inamtaka Osoro ambaye pia ni Kiranja wa Wengi Bungeni kuandikisha taarifa kuhusu anachokijua kuhusiana na ghasia za hivi majuzi jinsi alivyofanya Arati.
Mbunge huyo wa awamu ya pili, hata hivyo, amekana madai hayo.
Macho yote sasa yataangazia mashauriano hayo kuona ikiwa yatazalisha matunda yoyote na iwapo Machogu atamjibu Bw Arati kuhusu madai yake mapya dhidi ya Waziri huyo.