• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Baada ya bunduki za jeshi kushindwa wakazi wageukia maombi kupiga vita ujangili

Baada ya bunduki za jeshi kushindwa wakazi wageukia maombi kupiga vita ujangili

NA OSCAR KAKAI

KUFUATIA ongezeko la visa vya mauaji, uvamizi wa mara kwa mara na wizi wa mifugo katika eneo hatari lenye utata la Bonde la Kerio, viongozi wa kidini kutoka kaunti ya Pokot Magharibi wanajiandaa kufanya maombi maalumu katika maeneo ambayo hushuhudia utovu wa usalama.

Zaidi ya watu 20 wameuawa, mamia ya wakazi kupoteza makao na mali kuharibiwa katika eneo la Bonde la Kerio tangu mwaka huu uanze.

Viongozi hao ambao wako tayari kuanza misafara ya amani, kuandaa mikutano na waliokuwa wezi wa mifugo kisha wakazi ili kuimarisha na kudumisha amani wataombea waathiriwa wa ujangili na wizi wa mifugo.

Vile vile, watawahusisha wale walioasi maovu hayo na wale ambao bado wanahusika na ujangili kama njia mojawapo ya kukomesha mauaji ya mara kwa mara na wizi wa mifugo katika eneo hilo hatari.

Viongozi hao wa kidini pamoja na wazee wa utamaduni watakutana, kushirikiana na kujadili kuhusu masuala muhimu ya amani, msamaha na mbinu mpya za kuinua jamii na makundi ya watu pamoja na kupinga ujangili na maovu mengine ambayo yanaharibu amani katika eneo hilo.

Kati ya maeneo hatari ambayo yanalengwa ni Chesegon, Turkwel, Kainuk na Kapedo.

Askofu wa kanisa la African Inland Church (AIC) eneo la Pokot David Kaseton anasema kuwa mashambulizi yamekuwa shida kubwa na tishio kwa amani na ni maombi tu ndio yatamaliza tatizo hilo.

Anasema kuwa pia wanalenga maeneo kama Masol, Sook, Kaurion na Uganda ambapo watajenga makanisa mapya.

“Tutatembea milima na mabonde kupeleka huko neno la Mungu hadi mashinani. Tunataka kupeleka maombi katika maeneo ambayo yameathirika sababu mashambulizi sasa yamezidi,” akasema.

Anasema kuwa kwa sasa wako na makanisa 300 eneo hilo na wanataka kuyapanua na kufungua mengine kwa huduma hiyo.

“Tunataka kuwa na chuo cha Bibilia mjini Kapenguria kuongeza kile kiko eneo la Kong’elai,” anasema.

Askofu Kaseton anasema kuwa makanisa yatashirikiana na serikali kuu na za kaunti kwa maendeleo ya eneo hilo na kuhamasisha wakazi kuhusu umuhimu wa elimu.

“Tunataka kuenda mashinani kuongea na waathiriwa wenyewe. Tunataka watueleze changamoto ambazo wanakumbwa nazo. Kuna baa la njaa na wakazi kukosa kufanya kilimo kutokana na kiangazi. Tutakuwa msitari wa mbele kupigana na ujangili. Tunataka jamii jirani kuishi kwa amani,” anasema.

Askofu mpya wa kanisa la AIC eneo la Pokot ambaye aliapishwa eneo la Karas, Simon Yotta anasema kuwa kuna haja ya jamii hasimu kuwa na msamaha.

Alisisitiza kuwa maombi ndio mbinu pekee ya kukabiliana na ujangili na wizi wa mifugo katika eneo hilo.

“Mashambulizi yameacha familia nyingi kwa mateso baada ya wapendwa wao kuuawa na mifugo kuibwa,” akasema Naibu huyo wa Askofu

Alisema kuwa makanisa na misikiti itaungana pamoja na kuandaa mazungumzo katika kaunti za Pokot Magharibi, Elgeyo Marakwet, Baringo, Turkana, Samburu na Laikipia.

“Tunataka eneo la kati ambapo tutakutana na kuwa na maombi maalumu. Tukiwa na maombi tutaweza kuwa na barabara, vituo vya afya na shule ambazo zitafunguliwa. Wakazi kutoka maeneo ya mbali mashinani wanafaa kuona mwangaza. Hivi tutaweza kukomesha utovu wa usalama,” alisema.

Anaongeza kusema kuwa wataandaa maombi ya mara kwa mara katika maeneo ambayo yameathirika.

 

 

  • Tags

You can share this post!

CJ Koome alivyozima maandamano ya mawakili

Mpango kusambaza vyakula kupunguza visa vya wanafunzi...

T L