Habari za Kaunti

Baada ya mbolea feki, wakulima sasa wanalia mbegu faafu za mahindi hazipatikani madukani

April 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA OSCAR KAIKAI

MAELFU ya wakulima katika kaunti za Bonde la Ufa wamelalamikia ukosefu wa mbegu za mahindi hasa katika msimu huu wa mvua na upanzi.

Wakulima sasa wanahofia kusambaziwa mbegu mbovu, kuchelewa kupanda na kupata mavuno duni hali ambayo huenda ikachangia baa la njaa mwishoni mwa mwaka huu.

Kaunti za Pokot Magharibi na Trans-Nzoia ni baadhi ya zilizoathirika zaidi huku wakulima wakilazimika kusafiri mwendo mrefu katika kaunti jirani wakisaka mbegu za mahindi bila mafanikio.

Bw Joseph Long’urosya, anasimulia jinsi alivyosafiri kutoka kijiji chake cha Mutua, Kaunti ya Trans-Nzoia hadi eneo la Makutano, Kapenguria, Kaunti ya Pokot Magharibi Ijumaa, akitumai kurejea nyumbani na mbegu za mahindi.

Hata hivo, Bw Long’urosya, anayepanda mahindi kwenye ekari tatu za shamba, amekosa kupata mbegu za mahindi na matumaini yake ya kupata mavuno tele msimu huu wa upanzi, yamedidimia.

“Nimeenda maduka yote lakini sijapata chochote. Mimi hupanda kilo 25 za mbegu lakini naona mara hii nitachelewa. Huwa ninapanda mbegu za mahindi aina 6213 lakini hazipatikani. Mwaka jana hakukuwa na shida na mbegu zilikuwa kwa wingi,” alisema.

Alisema kuwa amekuwa akienda kutafuta mbegu mara kwa mara katika mji wa Kapenguria na Kitale wiki hii nzima bila mafanikio.

Kulingana na wakulima, udongo katika kaunti ya Pokot Magharibi huzalisha mbegu ya mahindi aina ya 6213,614 na 629 pekee.

Hata hivyo, udadisi uliofanywa na Taifa Leo katika maduka ya kuuza mbegu mjini Kapenguria, Pokot Magharibi hakuna aina ya mbegu hizo ambazo zinahitajika.

Hii imewafanya baadhi ya wakulima kuamua kupanda aina ya mbegu ya mahindi ya KH 500-43A na Pannar kutoka kampuni ya East African.

Aina nyingine ya mbegu ambazo zinapatikana ni DK &031, Pan 691, WH 5092, WH 101 na pioneer.

Mwenyekiti wa wakulima katika eneo hilo, Bw Richard Mwareng, alisema kuwa maduka ya kuuza mbegu katika eneo hilo hayajapokea mbegu za kutosha kutoka kwa kampuni ya Kenya Seed.

Bw Mwareng anayepanda mahindi eneo la Chepchoina na Kapenguria, alisema kuwa bado hajapanda mahindi.

Alieleza kuwa wakulima wanapata ugumu wa kupata mbegu kutoka kwa kampuni ya Kenya Seed, akisema kuwa alikaa siku mbili kwenye foleni kupata mbegu mjini Kitale na bado hakupata mbegu ya kutosha.