Habari za Kaunti

Baba katili achoma mwanawe wa miaka miwili na kutoroka

Na GEORGE ODIWUOR March 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MTOTO mwenye umri wa miaka miwili amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Homa Bay akiuguza majeraha baada ya kuchomwa na babake ambaye ametorokea mafichoni.

Mtoto huyo ambaye mama yake ni mwanafunzi wa Kidato cha Nne, alilazwa hospitalini humo mnamo Jumatano baada ya kuokolewa kutoka kwa ukatili wa babake.

Haijulikani kwa nini mzazi huyo alikuwa akilenga kumuumiza mwanawe.

Kwa mujibu wa ripoti ya daktari, mamake mtoto huyo alikuwa naye Jumapili babake alipofika kisha kumchukua na kuenda naye.

Mama huyo ambaye pia ni tineja aliamua kumsaka mwanawe maeneo jirani baada ya kumkosa.

Kwa mujibu wa nyanyake mtoto huyo, Bi Yago Agunga, walimpata mtoto huyo akiwa na majeraha ya kuchomwa moto mgongoni, babake naye akiwa ametoroka.

“Ilibidi tumpeleke hospitalini ili atibiwe na tulipata habari alionekana na mshukiwa (babake),” akasema Bi Agunga.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Homa Bay, Dkt Vincent Oduor, alisema mtoto huyo alijeruhiwa vibaya na sasa anashughulikiwa na madaktari wataalamu wa upasuaji.

“Ni kesi nzito na mtoto hawezi kutembea,” akasema Dkt Oduor. Kesi hiyo iliripotiwa katika kituo cha polisi cha Rodi Kopany na polisi wanaendelea kumsaka baba huyo.

Hali hiyo imesababishia mama mtoto msongo wa mawazo na anaendelea kupata ushauri na nasaha kutoka kwa makundi ya wanawake.

Mkurugenzi wa Huduma za watoto Homa Bay, Bw Patrick Awino, alienda hospitalini humo Jumatano kumwona mtoto huyo na kuangalia hali yake.

Katika hospitali hiyo hiyo, mwanafunzi wa Gredi ya Nne anaendelea kutibiwa baada ya kupigwa na wenzake alipokabidhi majina yao kama waliokuwa wakipiga kelele darasani.

Alipigwa mnamo Januari 8 na hadi wakati huu bado hajapona.

Mtoto huyo mwenye umri wa miaka 10, ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya Nyasumbi, eneo la Lambwe ambako alikuwa kiranja katika darasa lao.

Baada ya maumivu kumzidi, aliletwa katika hospitali hiyo mnamo Februari 17 akiwa na majeraha miguuni na bado hawezi kutembea.