Babu aliyenajisi mjukuu wake alishwa kifungo cha maisha
MWANAMUME mwenye umri wa miaka 55 katika Kaunti ya Tana River amehukumiwa kifungo cha maisha kwa kumnajisi mjukuu wake, 11.
Hakimu Mkuu Mwandamizi katika Mahakama ya Hola, Bw Edward Too, alimpa Kenneth Jillo kifungo hicho baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha ushahidi tosha dhidi yake.
“Ni wazi kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa mara kwa mara, na hana huruma kwa mtoto aliyetekelezewa unyama,” akasema Bw Too.
Mahakama ilielezwa kuwa Jillo alimwomba mtoto huyo kuenda chumbani mwake kwa dai la kumsaidia kazi za nyumbani, kabla ya kutumia nafasi hiyo kumnajisi mara kadhaa.
Upande wa mashtaka kupitia wakili Elijah Oruko, uliwaita mashahidi wanne ambao walishuhudia katika kesi dhidi ya mshtakiwa.
Korti ilielezwa kuwa mshtakiwa alifanya kitendo hicho siku kadhaa kati ya Juni 2022 na Julai 17, 2023, huko Hola Kaunti ya Tana River.
Mahakama ilijuzwa kuwa mshtakiwa alitumia muda ambao nyanyake (mkewe mshtakiwa) mtoto huyo hakuwepo nyumbani kutekeleza uovu huo, na kisha kumwonya vikali asimueleze mtu yeyote la sivyo atamdhuru.
Hakimu Too alielezwa na mke wa mshtakiwa kuwa mtoto huyo alikuwa amechoka na dhuluma hizo na akaamua kumweleza dada ya nyanya yake, ambaye alimjuza kuhusu yaliyokuwa yakiendelea.
Baada ya wawili hao kumuuliza mshtakiwa kuhusu madai hayo, aliomba msamaha akikiri kutorudia tena kitendo hicho.
Walikuwa wamemsamehea kabla ya kugundua kuwa mshtakiwa alikuwa amerejelea tabia hiyo.
“Mjukuu wangu alinieleza kuwa babu alikuwa amerudi kwa tabia yake ya kumnajisi na wakati huu alikuwa na hasira,” akasema nyanya.
Msichana huyo alifikishwa hospitalini ambako ilibainika alikuwa amenajisiwa mara kadhaa.