Habari za Kaunti

Baraza la Abagusii lakemea kuchapwa kwa mama kaburini

Na WYCLIFFE NYABERI March 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

BARAZA la Wazee wa Jamii ya Abagusii limejitenga na kisa ambapo mwanamke kutoka Kaunti ya Nyamira alidhalalishwa kwa kuchapwa katika kaburi la mumewe kutokana na uamuzi wake wa kukataa kurusha udongo kwenye kaburi la marehemu.

Jinsi ilivyo kawaida katika jamii nyingi za Kiafrika, jeneza la mtu aliyefariki likishashushwa kaburini, ndugu, jamaa na marafiki wa karibu wa mwendazake hutakiwa kurusha udongo ndani ya kaburi hilo kama ishara ya kumpa buriani ya mwisho.

Lakini katika kijiji cha Kiambere, kata ndogo ya Mwongorisi Kaunti ya Nyamira, mwanamke kwa jina Mellen Mogaka alikwenda kinyume na matarajio ya wengi alipokataa kurushia mumewe udongo kwa sababu zisizojulikana.

Jambo hilo lilimsababishia kichapo cha mbwa kutoka kwa watu waliokuwa kwenye mazishi hayo, huku wakijaribu kumlazimisha amwage mchanga katika kaburi la bwanake.

Matukio yaliyojiri katika mazishi hayo ya Ijumaa wiki jana (Machi 18, 2025), yaliibua hisia kali miongoni mwa Wakenya baada ya video iliyonasa kudhalilishwa kwa mama huyo kusambazwa mitandaoni.

Kwenye video hiyo, mama huyo aliyekataa katakata kurusha udongo kwenye kaburi la mumewe, anaonekana akipokea mapigo kutoka kwa mwanamume aliye na mjeledi.

Mwanamume mwingine aliyevalia kofia nyeusi, anamshika mkono na kumketisha katika kaburi hilo huku waombolezaji wengine wakilizunguka kaburi.

Kadri video hiyo inavyozidi kucheza, idadi ya wanaume wanaomlazimisha arudishe mchanga kaburini inaongezeka.

Watu wengine wanauchota mchanga kutumia vijiko vya kulima na kuuleta karibu na mikono yake wakimshurutisha aumwage.

Wengine wanauchukua mchango huo na kumwekea mikononi lakini mama huyo anagaragara chini kwa uchungu asitake kufanya jambo analolazimishwa kufanya.

Aidha, sehemu nyingine ya kanda hiyo inaonyesha mama huyo akiburutwa kutoka kwa shamba la majani chai hata baada ya kudhihirisha wazi msimamo wake.

Akiongea na Taifa Leo mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Abagusii Araka Matundura alisema, tukio hilo la Nyamira ni la aibu na halina nafasi kabisa katika jamii ya sasa.

Mwenyekiti huyo alihoji kuwa licha ya kwamba ni sehemu ya mila na desturi za jamii za Kiafrika kufuata utaratibu wa kuurudisha udongo katika kaburi la marehemu, dunia ya sasa imebadilika sana na nafasi ya mwanamke katika jamii inazidi kupewa kipaumbele.

Bw Matundura anaongeza kuwa chini ya Katiba ya sasa ya Kenya, ambapo kila Mkenya anatambua haki zake, mtu hafai kulazimishwa wala kupokea kichapo cha aina hiyo kwa kukataa kufanya jinsi watu wengine wanavyotaka.

Mwenyekiti huyo alisadiki kuwa Bi Mogaka alikuwa na sababu zilizomfanya kukaidi mila hizo na akashauri kuwa watu wa karibu wa marehemu huyo wangetafuta mbinu mbadala za kusuluhisha mgogoro huo.

“Mama huyo bila shaka alikuwa na sababu za kuchukua uamuzi wa kukataa kurusha udongo kaburini. Sababu au matatizo aliyokuwa nayo yangetatuliwa mwanzo kabla ya kuchukua hatua nyingine. Dunia ya sasa imebadilika na si kama ilivyokuwa zamani. Sasa hawa waliamua kumnyorosha mama huyo na hili ninalipinga vikali,” Mzee Matundura aliambia Taifa Leo kwa njia ya simu.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa mojawapo ya maana za mwanamke kurusha udongo kwa kaburi la mwanamume aliyefariki kunamaanisha kuwa mwanamke huyo yuko tayari kusalia katika boma la marehemu.

Lakini alisema kuwa kuna wengi ambao hurudisha udongo huo lakini baadaye huondoka na hakuna kitu athari au laana zozote zinazowafuata.

“Tumeshuhudia wanawake wanaorushia waume wao udongo lakini mwishowe wanaondoka katika boma hizo na kuolewa upya. Hivyo, kumpiga mama huyo sampli ile hakusaidii chochote. Kukataa kwa mama huyo kurusha udongo ni jambo wazi kuwa hataki kusalia katika boma ya marehemu,” Bw Matundura alisema.

Akiongea na wanahabari nyumbani kwake katika Kaunti ya Narok, Bi Mogaka alisema alikuwa ameolewa na mume huyo kabla ya kifo chake lakini ndoa yao ilikumbwa na misukosuko iliyosababisha watengane kwa muda.

Lakini alipokea taarifa kutoka kwa wakwe zake kuwa bwana yake huyo wa zamani alikuwa ameaga dunia baada ya kuhusika kwenye ajali.

Hivyo, aliombwa aje nyumbani na watoto waliokuwa wamezaa naye kuhudhuria mazishi yake.

Kufikia sasa, watu watatu wamekamatwa kuhusiana na kudhulumiwa kwa mama huyo.