Habari za Kaunti

Bei za sukumawiki na vitunguu zapaa Kajiado

June 11th, 2024 2 min read

NA STANLEY NGOTHO

MIJI kadha katika Kaunti ya Kajiado inakabiliwa na uhaba mkubwa wa sukumawiki na vitunguu kwa kipindi cha wiki mbili sasa, wateja wakilazimika kununua kwa bei za juu.

Utashi wa bidhaa hizo umeongezeka licha ya uhaba unaohuhudiwa katika miji ya Kitengela, Ngong, Kiserian, na Ong’ata Rongai.

Uchunguzi wa Taifa Leo katika soko la rejareja la Kitengela mnamo Jumanne ulionyesha kupungua kwa mboga na vitunguu.

Hali ilikuwa hivyo kwa supamaketi tatu maarufu zinazouza mboga na matunda katika mji huo.

Kwenye supamaketi moja, mboga ilikuwa imeisha.

Katika vibanda vya mama mboga, bei za sukumawiki na mchicha ni kati ya Sh15 na Sh30 kwa kila matawi ya mboga yaliyofungwa pamoja.

“Wasambazaji wa mboga hawafiki kama kawaida na hata wakileta, ubora uko chini ya wastani. Hali hii imekuwepo kwa muda sasa,” alisema msimamizi wa supamaketi moja katika mji wa Kitengela.

Bi Jane Wambua, ambaye ni mchuuzi wa mboga, aliambia Taifa Leo kwamba usambazaji wa mboga ulipungua baada ya mvua kubwa iliyonyesha mnamo Mei 2024.

“Upungufu wa mboga umesababisha bei kupanda. Kwa kawaida mboga huathiriwa pakubwa na mvua kubwa. Mboga bado ni bidhaa adimu kwa sasa,” akasema Bi Wambua.

Mchuuzi mwingine wa mboga Bi Rachel Mundia, alisema kwamba gunia la kilo 70 za sukumawiki linauzwa kwa Sh3,000 bei ya jumla.

“Jumanne asubuhi na mapema nimenunua gunia la sukumawiki kilo 70 kwa Sh3,000. Unapaswa kuamka mapema ili kupanga foleni. Kiwango cha faida ni kidogo ikilinganishwa na miezi miwili iliyopita,” akasema Bi Mundia.

Hivi majuzi, mashamba ya mboga katika Kaunti Ndogo ya Mavoko karibu na Mto Athi yalifagiliwa na maji ya mafuriko yaliyoharibu mboga hizo.

Kwa miaka mingi Athi River imekuwa miongoni mwa sehemu za ukuzaji wa mboga zinazotegemewa na wakazi wengi wa Kitengela.

Bei za vitunguu nazo zimepanda kutoka Sh80 kwa kilo miezi miwili iliyopita hadi Sh150. Kitunguu kidogo kinauzwa kwa Sh10 ambapo walaji wanaumia pakubwa.

Bi Lydia Ndung’u ni muuzaji wa vitunguu mjini Kitengela. PICHA | STANLEY NGOTHO

Ikizingatiwa kuwa ugali kwa sukumawiki ni chakula kikuu kinachopendelewa zaidi na familia nyingi hasa mijini, uhaba wa sukumawiki umewaacha wakazi wengi wa mijini wakipambana na hali mbaya ya kupata mlo wa kila siku.

Bw James Kimani,55, dereva wa basi linalohudumu mjini Kitengela alisema bei ya sasa ya sukumawiki na vitunguu imeacha familia nyingi zikiumia.

“Siku hizi vifurushi vitano vya sukumawiki vinauzwa hata kwa Sh100. Ni vigumu kulisha familia ya watu watano kama hapo awali. Gharama ya maisha iko juu sana,” akasema Bw Kimani.

Hali hii imefaanya baadhi ya wauzaji wa mboga katika eneo hilo kufunga biashara hiyo kwa muda.