Habari za Kaunti

Biashara ya kumbi za kijamii yanoga mji wa Mokowe ukipanuka

February 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA KALUME KAZUNGU

WAWEKEZAJI mjini Mokowe wameibukia biashara ya kujenga na kukodisha kumbi za kijamii ambayo inaonekana kufanya vyema siku za hivi karibuni.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Jumapili ulibaini kuwa wajasiriamali wengi wanapendelea kuwekeza kwenye ujenzi huo wa kumbi za kijamii, wakikiri kuwa biashara hiyo ‘ndiyo kusema’ kwa sasa eneo hilo.

Ikumbukwe kuwa hadhi ya mji wa Mokowe inaendelea kupanda, hasa tangu makao makuu ya serikali ya kaunti ya Lamu na ofisi ya kamishna wa eneo hilo kuhamishwa kutoka kisiwa cha Lamu hadi mjini humo karibu miaka mitatu iliyopita.

Isitoshe, kukamilika na kufunguliwa rasmi kwa Bandari ya Lamu (Lapsset) na serikali kuu mnamo Mei 20,2021 ni miongoni mwa vigezo vinavyoendelea kuunawirisha mji wa Mokowe na viunga vyake, hasa kibiashara na maendeleo.

Baadhi ya wawekezaji waliohojiwa walisema ni kupitia biashara ya kumbi za kukodisha za kijamii ambapo fedha za haraka hupatikana.

Mohamed Kassim Shahareambaye ni mwekezaji mmiliki wa mkahawa wa Mokowe Islanders Point Restaurant, anasema mbali na hoteli, yeye pia aliafikia kujenga ukumbi wa kijamii.

Bw Shahare anasema ofisi nyingi za serikali zilizoko Mokowe ndizo zinazotegemewa kwa wateja wanaokodisha kumbi hizo za kijamii, iwe kwa mikutano au shererehe za kiofisi.

Anataja kuwa baadhi ya wafanyakazi wa serikali wanaoishi Mokowe pia wamekuwa wakikodisha kumbi hizo kwa sherehe za kibinafsi, ikiwemo kukumbuka siku zao za kuzaliwa, zile za kuleta wafanyakazi marafiki pamoja na nyinginezo.

Watu wakiwa katika ukumbi wa kijamii wa Mokowe wakiwa wamekalia viti vya samawati. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Shahare anasema malipo ya kukodisha ukumbi wa kijamii, iwe ni kwa masaa au siku huanzia kati ya Sh10,000 hadi Sh20,000.

“Biashara ya kukodisha kumbi za kijamii zinazotumika kuandalia mikutano imechipuka kweli hapa Mokowe japo wateja bado ni finyu. Ofisi zilihamishiwa hapa miaka ya hivi majuzi, hivyo wafanyikazi bado wanajipanga. Kama wawekezaji, tuko mbioni kujiandaa mapema kwa kujenga kwa wingi hizi kumbi za kijamii tukijua fika kuwa mwisho wa siku mikutano mingi ya kiofisi na ile ya kijamii itakuwa ikifanyika hapa Mokowe,” akasema Bw Shahare.

Bi Beatrice Mwangi, mmoja wa wawekezaji, pia alisifu kupanda kwa hadhi ya mji wa Mokowe, akitaja kuwa jambo zuri kwao, hasa kibiashara.

Bi Mwangi anasema anatarajia eneo hilo kunoga zaidi kibiashara, hasa ikizingatiwa kuwa Bandari ya Lamu tayari inaendeleza shughuli zake tangu kufunguliwa kwake rasmi 2021.

“Kuna ofisi za Lapsset ambazo zimejaa wafanyakazi eneo la Kililana, karibu na Mokowe. Bunge la kaunti ya Lamu pia limehamishiwa hapa. Ofisi za mashirika mbalimbali, ikiwemo utafiti wa misitu (Kefri), ya mazingira (Nema) na nyinginezo piazipo hapa Mokowe. Tunatarajia mikutano ya kila mara kufanyika kwenye kumbi hizi zetu za kijamii, hivyo kujipatia mtaji,” akasema Bi Mwangi.