Habari za Kaunti

Bodaboda watishia kuchukua sheria mkononi polisi wasipozima wezi

May 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA LUCY MKANYIKA

VIONGOZI wa Kaunti ya Taita Taveta wametishia kuchochea wahudumu wa bodaboda katika kaunti hiyo kuchukua sheria mkononi ikiwa polisi hawatakomesha mauaji ya wahudumu na wizi wa pikipiki katika eneo hilo.

Viongozi hao walikuwa wakiongea wakati wa mazishi ya mwendeshaji bodaboda Silo Mwachongo aliyepoteza maisha yake mikononi mwa wezi wa pikipiki wiki jana katika eneo la Voi.

Wakati wa mazishi hayo yaliyofanyika katika kijiji cha Chakakeri, eneo la Mwatate, viongozi hao walitoa onyo kali kwa polisi na wezi wanaohusika na wizi wa pikipiki, ambao umekuwa ukiendelea bila kukomeshwa.

Jeneza lililobeba mwili wa mwendeshaji bodaboda Silo Mwachongo wakati wa ibada katika steji ya Voi, Taita Taveta. Waendeshaji bodaboda wameapa kuchukua sheria mkononi ikiwa polisi watashindwa kukomesha vifo vya wahudumu hao. PICHA | LUCY MKANYIKA

Hali ya simanzi iligubika waliohudhuria mazishi hayo huku kitendo hicho kikilaaniwa vikali na kidole cha lawama kikielekezwa kwa polisi kwa kile walidai ni kuzembea katika kutekeleza majukumu yao ya kuhakikisha usalama na maisha ya wenyeji.

Hii ni mara ya pili kwa kipindi cha mwezi mmoja ambapo jamii ya wahudumu wa bodaboda inapoteza mmoja wao kwa njia ya kikatili.

Mwezi Aprili mhudumu mwingine aliuawa katika eneo hilo na tangu mwaka huu 2024 kuanza, jumla ya pikipiki tano zimeibiwa.

Mbunge wa Mwatate Peter Shake alisema kuwa wahudumu wa bodaboda wamekuwa wakilalamika kuhusu kudorora kwa usalama na wizi unaoendelea, ambao umewaacha wengi wao bila kazi na wengine kupoteza maisha.

“Pia mimi nashutumu visa hivi kwa sababu kwa nini kusiwe na usalama wa wananchi wetu? Polisi wanafaa kuamka na kutekeleza majukumu yao ili kulinda maisha na hatutakubali watu kuawa kiholela,” alisema Bw Shake.

Alisema sekta ya bodaboda ni muhimu kwa uchumi wa nchi na hivyo ipo haja ya kuhakikisha usalama wao.

“Ikiwa polisi walioko huku hawatatekekeza kazi yao basi waondolewe waletwe wale wanaoweza kutoa ulinzi,” alisema.

Aliwataka wahudumu wa bodaboda kuwa waangalifu wanapotekeleza kazi zao.

Vilevile, mwakilishi wa wadi ya Kaloleni, Azar Din, alisema kuwa ikiwa polisi watashindwa kutekeleza wajibu wao wana bodaboda watajilinda wenyewe.

“Wakati wa mazishi yaliyopita tulitoa onyo kwa polisi kuwa washike washukiwa waliotekeleza kisa hicho. Ni masikitiko makubwa kuwa leo pia tunazika kijana mdogo aliyeuliwa na majambazi licha ya kuwa na maafisa wa usalama katika eneo hili. Sasa imefika kipindi cha sisi wenyewe kuchukua hatua,” akasema Bw Din.

Mwenyekiti wa bodaboda wa Voi, Paul Chege, aliwataka polisi kukoma kuwakamata kiholela na badala yake kufanya uchunguzi wa kina ili kuwatambua na kuwakamata wahalifu halisi.

“Tumechoka kuzika ndugu zetu. Tumechoka kuibiwa pikipiki zetu ambazo ni riziki yetu. Sasa tutawasaka hawa wezi na wauaji na kuwafunza adabu wenyewe,” akasema Bw Chege.

Aliapa kuwa iwapo polisi hawatachukua hatua za haraka, basi wao kama jamii ya wanabodaboda, watachukua sheria mikononi mwao.

“Polisi wanapaswa kutambua kwamba sisi si adui. Sisi ni raia wema tunaotafuta riziki yetu kwa njia halali. Tunataka haki itendeke na usalama wa pikipiki zetu uhakikishwe,” alisema.

Mwenyekiti wa wahudumu hao katika ngazi ya kaunti, Bw Mohammed Dudu, ambaye pia ni diwani maalum wa bunge la kaunti hiyo, alisema kuwa jamii ya bodaboda inaitaka serikali kuingilia kati na kuhakikisha kwamba kuna mikakati madhubuti ya kuzuia wizi wa pikipiki na kuimarisha usalama wa wahudumu wa bodaboda.

“Tunaomba ushirikiano baina ya polisi na wana bodaboda ili kuleta suluhu ya kudumu kwa tatizo hili linaloendelea kuwa tishio kwa maisha na riziki yetu,” alisema Bw Dudu.