Habari za Kaunti

Bunge kulipa Sh900,000 kwa kuanika Wasifu Kazi wa mwaniaji

Na SAM KIPLAGAT, BENSON MATHEKA October 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

BUNGE la Kaunti ya Migori limeagizwa kulipa mwaniaji wa kiti cha Spika katika gatuzi hilo Sh900,000 kwa kukiuka haki yake ya faragha baada ya kuchapisha Wasifu Kazi wake kwenye tovuti kinyume cha sheria.

Bw Allan Chacha alituma maombi ya kuwa Spika wa Bunge la Kaunti ya Migori mnamo Mei 2024, lakini hakufaulu, na akawasilisha malalamishi hayo katika Afisi ya Kamishna wa Data baada ya wasifu wake kutangazwa hadharani.

Bw Chacha alisema licha ya kupoteza wadhifa huo, bunge la kaunti lilichapisha na kuhifadhi Wasifu kazi wake kwenye tovuti, ambao una habari muhimu za kibinafsi.

“Kwa hivyo, bunge la kaunti ya Migori halikuwa na msingi halali wa kuchapisha wasifu wa mlalamishi kwenye tovuti yake na kuufanya upatikane na watu ambao si wanachama wa Bunge la Kaunti ya Migori,” Kamishna wa Data, Bi Immaculate Kassait alisema.

Aliagiza wasifu kazi huo ufutwe ndani ya siku saba kuanzia tarehe ya uamuzi.

Bunge la kaunti lilijitetea likisema lilitumia kanuni za kudumu kuchapisha wasifu kazi huo kwani unafaa kutolewa kwa madiwani wa bunge la kaunti.

Bi Kassait, hata hivyo, alikataa upande wa utetezi akisema Kanuni za Kudumu zinasema kwamba ni orodha tu ya walioteuliwa ndiyo inayopaswa kuwekwa wazi.

Kamishna wa Data alibainisha kuwa ukaguzi wa tovuti kutoka mabunge mbalimbali ya kaunti kote nchini ulifichua kuwa ni orodha tu ya walioteuliwa iliyochapishwa bila wasifu kazi wao.

“Hivyo basi, mlalamishi ana haki ya kufidiwa. Mshtakiwa anaagizwa kulipa mlalamishi Sh900,000,” alisema Bi Kassait.

“Kwa kufanya hivyo, ofisi hii inazingatia asili ya data ya kibinafsi iliyofichuliwa kuwa data muhimu ya kibinafsi, ukweli kwamba ilichapishwa katika tovuti inayopatikana na umma,” alisema.

Bi Kassait alisema kifungu cha 25 cha Sheria kinahakikisha kwamba data ya kibinafsi inashughulikiwa kwa mujibu wa haki ya faragha ya mwenye data.

Sheria hiyo pia inasema kwamba mdhibiti au anayeshughulika na data atahakikisha kwamba data inakusanywa kwa madhumuni ya wazi, yaliyobainishwa na halali na haitatumiwa kwa njia isiyolingana na madhumuni hayo.

Kamishna wa Data alibainisha kuwa wasifu huo ulikuwa na jina kamili la Bw Chacha, nambari ya kitambulisho, nambari ya simu na taarifa kuhusu watu aliotaja kuwa wadhamini wake.

Data muhimu za kibinafsi ikiwa ni pamoja na imani yake ya kidini na hali ya ndoa pia ilikuwemo kwenye stakabadhi hiyo na ilitolewa kwa umma.

Kamishna huyo alisema kitendo cha kuweka wasifu kazi hadharani kwenye tovuti yake ni kinyume na madhumuni na haki yake ya faragha.