Habari za Kaunti

Bungoma yavuna minofu kabla ya Madaraka Dei

May 30th, 2024 1 min read

NA JESSE CHENGE

HUKU Kaunti ya Bungoma ikijiandaa kuwa mwenyeji wa Makala ya 61 ya sherehe za kitaifa za Madaraka Dei, wakazi wanashuhudia maendeleo yanayofanywa haraka upesi.

Kulingana na Halmashauri ya Barabara za Mijini (Kura), Bungoma imepata maendeleo ya upanuzi wa hadi kilomita 21 za barabara.

Mkurugenzi Mkuu wa Kura, Bw Silas Kinoti, ambaye alikuwa kwenye ziara ya ukaguzi wa barabara mjini Bungoma, alisema kazi hizo zilifanywa kwa gharama ya takriban Sh1.8 bilioni.

Barabara hizo zitasaidia sana mji wa Bungoma ambao ni kitovu na njia muhimu kwa bidhaa zinazoenda au kutoka Uganda na maeneo mengine.

“Ukarabati na ujenzi wa barabara huchangia pakubwa katika kuimarisha viwango vya maisha ya watu. Isitoshe, husaidia kufungua upatikanaji wa huduma muhimu na kuimarisha usalama,” Bw Kinoti alisema.

Aliongeza kuwa barabara zina jukumu muhimu katika kujenga imani kwa wawekezaji na kuwaunganisha watu.

“Barabara hizi zitaimarisha uwezo wa Bungoma na eneo la Magharibi katika uundaji wa nafasi za kazi na kukua kwa miji,” akaongeza.

Chini ya mpango wa serikali kuruhusu wanakandarasi kuchora dizaini za barabara na kujenga huku ikiwalipa kwa awamu, Kura imesimamia ujenzi wa mtandao wa barabara unaofikia jumla ya kilomita 14.7. Hizi barabara ni pamoja na barabara ya C33 ya Bungoma-Mateka-Samoia-Muslim Primary yenye urefu wa kilomita 6.3.

Pia kuna barabara ya A104 ya Mateka-Mwanda-Siritanyi, ambayo ni ya kilomita 8.4.

Aidha, Kura imefanya ukarabati wa barabara kadhaa ambazo kwa ujumla ni za umbali wa kilomita 6.5 ndani ya mji wa Bungoma kama maandalizi ya sherehe za Madaraka Dei.

Barabara hizo ni zile za kuingia katika uwanja wa Masinde Muliro Kanduyi, barabara ya Shule ya Upili ya Wamalwa-Kijana, Elegant Road, Kanduyi DEB-Lusaka Road, barabara ya West FM Loop, na Khetias Back Street.

Barabara hizi zitawanufaisha wakazi wa Bungoma pamoja na miji mingine jirani ndani ya eneo la Magharibi.

Ili kufanikisha ujenzi huu wa barabara, sekta hiyo imepigwa jeki kupitia uwekezaji wa kifedha.