Habari za Kaunti

Bustani ya Uhuru Park yafungwa tena kufuatia maandamano ya Gen Z

Na KEVIN CHERUIYOT na WINNIE ONYANDO August 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

BUSTANI ya Uhuru Park imefungwa tena kutokana na uharibifu mkubwa uliotokea wakati wa maandamano ya vijana wa Gen Z.

Japo serikali ya Kaunti ya Nairobi na ile ya kitaifa hazijatoa kiasi kamili cha hasara iliyokadiriwa wakati wa maandamano ya vijana hao, Uhuru Park na Central Park zitafungwa ili kutoa nafasi kwa serikali kufanya ukarabati.

Maandamano hayo ya kukosoa serikali ya Rais William Ruto, yalianza miezi miwili iliyopita.

Bw Ibrahim Otieno, ambaye ni Afisa wa kaunti anayesimamia masuala ya Mazingira, alisema kuwa bustani ya Uhuru itafunguliwa baada ya serikali kufanya ukarabati.

Lango la kuingia kwenye bustani hiyo liliharibiwa.

Kando na hayo, ndege ya zamani ya Boeing 737 ambayo ilikusudiwa kutumika kama mkahawa na kituo cha burudani iliteketezwa na hata vifaa vingi, vikiwemo vyoo viliharibiwa.

“Waliharibu vyoo vyote na kuteketeza basi. Uharibifu ulikuwa mkubwa sana,” Bw Otieno aliambia Taifa Dijitali.

Bustani hilo lilifunguliwa upya na Gavana Johnson Sakaja wa Nairobi Machi mwaka huu, 2024.

“Muundo mpya wa bustani hili utatoa nafasi kwa Wakenya wa tabaka mbalimbali kufika na kufurahia mandhari ya kipekee jijni,” Bw Sakaja alisema alipokuwa akifungua rasmi bustani hilo.