Habari za Kaunti

Daraja la mbao lililotengenezwa na mkazi laokoa wanaohepa barabara mbovu Nyatike

Na GEORGE ODIWUOR January 19th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

DARAJA ndogo la miti lililotengenezwa na James Odhiambo kusaidia watoto wake kuvuka mto katika wadi ya Kadem Kaskazini, Kaunti ya Migori sasa linawasaidia wenye magari wanaosafiri kutoka Sori kuenda mjini Migori.

Walipoanza kutumia daraja hilo Desemba mwaka jana, wenye magari hao walisema walifikia uamuzi huo baada ya kuchoshwa na hasara ya kuharibika kila mara kwa magari yao wakitumia barabara mbovu kati ya kituo cha kibiashara cha Lwanda na Nyakweri.

Hii ni baada ya habari kuenea katika kijiji cha Kuoyo Majiwa kwamba daraja hilo kwa jina, “Angugo ” lilikuwa thabiti licha ya kutengenezwa kwa mbao na miti na Bw Odhiambo, miaka miwili iliyopita.

“Watu wengi wanaoenda sokoni hupendelea kutumia daraja hili kwa sababu inawafupishia safari. Mwanzoni, lilitumiwa na watu kutoka eneo hili pekee, hadi wafanyabiashara walipoanza kulitumia kwa kuchoshwa na ubovu wa barabara ya kawaida,” akaeleza Yunia Owino, ambaye ni mmoja wa wale walioanza kufaidi kwa kutumia daraja hilo.

Lakini matumizi ya “Angugo B” sasa yamechukua mwelekeo wa kisiasa katika eneo bunge la Nyatike wakazi wakimkosoa mbunge, Tom Odege, kwa kushindwa kutekeleza mradi huo “ilhali raia wa kawaida Bw Odhiambo ameifanikisha.”

Wapinzani wa Mbunge huyo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 sasa wanatumia daraja hilo kumpiga vita Bw Odege.

Barabara ya kutoka Sori kuendaa mjini Migori, kupitia Masara, iko katika hali mbaya zaidi. Ina mashimo mengi, hasa sehemu ya kati mwa kituo cha kibiashara cha Lwanda na Nyakweri.

Wakazi wanasema kuwa barabara hiyo ni mbovu kiasi kwamba wahudumu wa pikipiki wanaweza kupotelea ndani ya mashimo fulani.

Wakazi wanasema, ubovu wa barabara hiyo umeongezwa na shughuli za uchimbaji mchangarawe zinazoendeshwa katika eneo hilo; mojawapo ya kitega uchumi katika eneo hilo.

“Hii ndio barabara ya kipekee tunayo. Hali yake ni mbaya zaidi kiasi kwamba tunapitia changamoto nyingi tunapoitumia. Serikali inasema inaifanyia ukarabati, lakini kazi hiyo haijafikia eneo hilo, akasema Tom Ocholla, mkazi.

Baada ya idadi ya magari yanayotumia daraja la Angugo kuongezeka, Bw Odhiambo aligundua nafasi yake ya kujichumia pato kutokana na jasho lake alipolijenga daraja hilo.

Alianzisha ada kidogo ya Sh50 kwa magari na Sh30 kwa pikipiki.

Bw Odhiambo aliweza kupata pesa nyingi kwa siku kutokana na utozaji wa ada hizo.

Taifa Leo ilipozuru kituo cha ukusanyaji ada hizo, mwanamke fulani alikuwa akikisimamia.

“Watu hulipa mara moja tu kwa siku. Baadhi ya magari hupita hapa mara nyingi kutokana na biashara zao. Ninalazimika kukumbuka nyuso zao ili nisiwatoze zaidi ya mara moja,” alieleza.

Magari ya uchukuzi aina ya Toyota Probox ambayo hubeba abiria 10 kupita katika daraja hilo kwa urahisi zaidi.