Dennis Onsarigo ajiuzulu kazi Nyamira akilalamikia ubovu wa vyoo
NA WYCLIFFE NYABERI
MWANAHABARI Dennis Onsarigo aliyejizolea umaarufu kwa kuangazia maswala ya uhalifu, amejiuzulu kutoka kwa wadhifa wake wa mkuu wa wafanyakazi katika serikali ya Kaunti ya Nyamira.
Bw Onsarigo aliteuliwa katika nafasi hiyo mnamo Oktoba 2022 na Gavana Amos Nyaribo lakini amedokeza kuwa hakupewa nafasi nzuri kutekeleza majukumu yake.
Kwenye barua aliyomwandikia mkubwa wake, Bw Onsarigo alisema mojawapo ya sababu zilizomfanya kujiendea zake ni kwamba alijaribu kumtafuta gavana Nyaribo ili wajadili jinsi ambavyo wangeweza kushirikiana ili amwezeshe kufanikisha ajenda zake kwa raia lakini juhudi hizo zilifeli.
“Jinsi ujuavyo, nilijaribu mara nyingi kukutana nawe tujadili kwa kina jinsi ambavyo afisi yangu ingeshirikiana na wewe ili kufanikisha manifesto yako. Lakini hilo halikufanyika,” imesema sehemu ya barua ya Bw Onsarigo, yenye kurasa mbili na nusu na ambayo alitia saini mnamo Januari 10, 2024.
Ofisi ya Gavana iliipiga muhuri barua hiyo mnamo Januari 24, 2024.
Mwanahabari huyo alifichua kwamba hakufurahishwa na kitendo kingine cha walinzi na madereva wa gavana Nyaribo kutolipwa marupurupu yao kwa miezi kadhaa, licha ya kwamba pesa zao zilikuwa zikitolewa na Mdhibiti wa Bajeti (CoB).
Kushangaza zaidi, Bw Onsarigo alidokeza kuwa afisi ya sasa ya gavana Nyaribo haikuwa na vyoo vyenye ubora unaostahili kwa gavana na aghalabu waliona aibu kila wakati walipotembelewa na wageni wengi ambao pia alisema hawakuwa wanatosha katika sehemu ya mapokezi kwani ile ya sasa ni ndogo.
“Mpango wa kuikarabati afisi yako na kuijengea vyoo vya kisasa ili vituondolee fedheha tuliyokuwa tukiipata wakati wageni wengi walikuwa wakitutembelea haukuwezekana pia. Vyoo vya sasa haviashirii ishara yoyote ya kuitwa vyoo kwa kuwa hakuna maji ya kutosha na vifaa vingine vinavyotumika humo ndani. Choo cha sasa kinawafaa tu wanaume na wageni wanawake wanaotutembelea hupata wakati mgumu kuvitumia,” Bw Onsarigo aliongeza.
Pia mwanahabari huyo aliongeza kuwa afisi yake ilikuwa imeanza kupata pingamizi na baadhi ya watu waliwasawiri kama wale waliokuwa wakilenga kupora pesa za umma.
Isitoshe, alidai pia baadhi ya vijana waliokuwa wakitafuta kazi katika serikali ya Nyamira, walikuwa wakishinikizwa kutoa hongo ndiposa wazingatiwe kwa ajira zozote.
“Licha ya bidii kutoka kwa idara yangu, imebainika kuwa changamoto tunazozipitia hatuwezi tukastahimili zaidi ya hapo na kwa hivyo, kuendelea kwangu kuhudumu katika wadhifa huu hakutakuwa kwema kwa maendeleo tunayopania. Nilieleza hofu zangu kwako lakini sitataka ifikie kiwango ambapo nitaonekana kuwa sina uwezo wa kufanya kazi yangu,” akasema huku akimshukuru Bw Nyaribo kwa muda huo aliomteua afisini.
Mnamo Februari 2022, Bw Onsarigo aliteuliwa kusimamia mawasiliano katika kampeni za kinara wa Orange Democratic Movement Raila Odinga, aliyewania kiti cha urais mwaka huo.
Kabla ya kujiunga na kambi ya Bw Odinga, Bw Onsarigo aliyeondoka katika kituo kimoja cha runinga humu nchini mwaka 2018, alifanya kazi katika Kaunti ya Taita Taveta kama afisa wa mawasiliano pia.