Dereva alivyotumia kazi za masomo za mwanawe kupata D+ KCSE
MWANAUME mmoja katika Kaunti ya Homa Bay, alijinufaisha kimasomo kutokana na kazi za ziada ambazo mwanawe alikuwa akitumiwa na walimu wake kujiandaa kwa mtihani wa kidato cha nne (KCSE) na akafanikiwa kupata gredi ya D+.
Bw George Ochieng Okumu, 50, ambaye ni dereva wa gari la uchukuzi aina ya Probox, kutoka Homa Bay na mwanawe wa kiume Brennon Arsen Ochieng alikuwa mwanafunzi katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Orero iliyoko eneobunge la Rangwe.
Ochieng’ alikuwa akitumiwa kazi za masomo mbalimbali na walimu wao kupitia mtandao wa WhatsApp katika simu yake na hivyo ndivyo baba yake Bw Okumu alizitumia kujiandaa kwa KCSE 2025, sambamba na mvulana huyo.
Brennon alipata gredi ya B-.
Wakati huo huo, walimu Jumapili walivuruga na kutibua uchaguzi wa Muungano wa Walimu wa Shule za Upili na Vyuo Anuwai (KUPPET) Homa Bay, kambi tofauti zikingángánia uongozi.
Kwa kawaida, walimu hutarajiwa kuwa watu wenye nidhamu na kielelezo chema au bora kwa wanafunzi.
Hata hivyo, hilo waliliweka kando, wakachukua masanduku ya kupiga kura kutoka eneo la kupiga kura na kuteketeza karatasi za kupiga kura.
Vurugu hizo zilisababisha uchaguzi huo kutibuka na hakuna washindi waliotangazwa huku mtu mmoja akijeruhiwa.
Hata uwepo wa Katibu wa Kuppet Akelo Misori katika Chuo Kikuu cha Tom Mboya ambako uchaguzi huo ulikuwa ukiendelea, haukuwahofisha walimu hao na kusababisha waachane kwa fujo hizo.