Habari za Kaunti

Dhehebu potovu laibuka tena Kilifi polisi wakipekua kubaini hatima ya watoto 6

Na MAUREEN ONGALA July 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

POLISI katika Kaunti ya Kilifi wanachunguza iwapo kundi la imani potovu lililonaswa mwishoni mwa wiki katika eneo la Binzaro, lina uhusiano na dhehebu la Shakahola ambalo lilisababisha vifo vya zaidi ya watu 400.

Boma ambalo mwanamume alipatikana amefariki na watu wengine wanne wakiwa katika hali dhaifu Jumamosi, liko karibu kilomita saba kutoka barabara kuu ya Malindi–Sala Gate.

Ndani ya boma hilo kuna nyumba tatu zilizojengwa kwa udongo na paa za mabati lakini hazina madirisha yoyote. Kuna bwawa la maji ambalo halijakamilika kujengwa, banda la kuku, na eneo la kupikia nje.

Mahali hapo hakuna vitanda, jambo ambalo linaashiria kuwa wakazi walilala sakafuni. Choo kinachoonekana kama banda dogo kilichofichwa katika vichaka karibu na lango kuu, kuashiria mazingira magumu kwa wakazi.

Sehemu mbalimbali za ardhi zilikuwa zimevurugwa na hivyo kuibua hofu ya kuwepo kwa makaburi, jambo ambalo maafisa wa polisi sasa wanajaribu kuthibitisha.

Wapelelezi walimkamata mshukiwa mkuu wa kundi hilo Jumapili.

Kamishna wa Kaunti ya Kilifi Josephat Biwott, alisema mshukiwa huyo mwanamke, ambaye polisi bado hawajatoa jina lake rasmi kwa umma, alikamatwa Kisauni, Kaunti ya Mombasa.

Kukamatwa kwake kulifikisha idadi ya watu walio kizuizini kuwa 11.

Miongoni mwao ni watu wanne waliookolewa kutoka boma hilo, wanne waliokamatwa Kisauni, na watatu wanaoaminika kumuuzia ardhi mshukiwa mkuu.

“Wako chini ya ulinzi wa maafisa wa DCI (Idara ya Upelelezi wa Jinai) kwa ajili ya uchunguzi. DCI wanaenda mahakamani kuomba kibali cha kuweka ulinzi katika eneo hilo, kusaka muda wa uchunguzi zaidi na kufukua miili ikiwa itahitajika,” Bw Biwott alieleza na kuongeza kuwa waliookolewa watatakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu hatima ya watoto waliokuwa nao.

Wakazi wa kijiji cha Binzaro wameeleza kuwa mwenye boma ni mgeni aliyeonekana akitafuta ardhi hivi majuzi. Mnamo Machi alifika kwa mmoja wa wakazi akitafuta kipande cha ardhi anunue.

Mkazi mmoja Sara Thoya alieleza jinsi mumewe aliuza sehemu ya shamba lao la ekari tano kwa Sh18,000 kwa mwanamke huyo mshukiwa.

“Nilikuwa nyumbani mume wangu akaja kuniambia kuna mwanamke anayetaka ardhi, na kuomba auze sehemu ya kipande changu lakini nilimwambia auze ya kwake. Tulimpa chakula cha mchana lakini alikataa na kusema alikuwa anafunga,” alieleza Bi Thoya.

Mkazi mwingine Bi Kanze Kenga alisema mwanamume ambaye baadaye alitambuliwa kama Bw Jairus Otieno alimwendea kuomba usaidizi.

Bw Otieno, ambaye aliripotiwa kupotea Kaunti ya Siaya mwezi Aprili, alikuwa amehamia Binzaro pamoja na mkewe na watoto wao sita. Hadi sasa haijulikani walipo watoto hao.

Alienda kwa Bi Kenga kuomba simu ya mkononi ili awasiliane na familia yake.

Hatua hiyo ndiyo ilipelekea kufichuka kwa mambo yaliyokuwa yakiendelea katika boma hilo.

“Alipiga namba mbili ila wenyewe walikuwa mteja. Alijaribu namba ya tatu na akafanikiwa kuwasiliana na aliyepokea. Aliniambia alikuwa anatoka msituni na alikuwa akisubiri kaka yake amchukue. Alikuwa dhaifu mno na nilipoweka chakula mbele yake alikataa kula,” Bi Kenga alieleza.

Kaka wa Bw Otieno baadaye alipiga simu kwa Bi Kenga akiwa na wasiwasi.

“Kakake alinipigia kuuliza iwapo Jairus bado alikuwa hapo. Nikamwambia aliondoka. Kisha akasema alikuwa kwenye shida kubwa. Nilipomuuliza ni shida gani akasema kuna watu wanamfuata kutoka Shakahola,” aliongeza Bi Kenga.

Baada ya mawasiliano hayo ya simu jamii ilichukua hatua ikawazuilia wanawake wawili, ambao baadaye walikiri kwamba walikuwa wametoroka kutoka kwa boma la mshukiwa mkuu.

Mkazi mwingine Bw Kahindi Beja alisema wanajamii wamekuwa wakitilia shaka visa vya vifo eneo hilo katika miezi michache iliyopita wakidhani vilisababishwa na tembo waliotoka misituni.

Kwa mujibu wake, wakazi waliamini vifo hivyo vilisababishwa na tembo waliotoka misituni.

Alieleza kuwa wafugaji mara kwa mara walikuta mifupa ya binadamu na miili vichakani, lakini waathirika hawakuwahi kutambulika wala kuripotiwa kupotea.

“Ni mtoto wake wa mwisho alimsababisha kutafuta msaada. Alisema mtoto alichukuliwa usiku akipelekwa msituni na alikuwa akilia akimwita baba yake. Alipojaribu kufuata, alikutana na wanaume waliomzuia na tangu siku hiyo hajawahi kuonekana tena,” alisema Bw Beja.

Wapelelezi wamethibitisha kuwa, mwili uliopatikana humu ulikuwa wa mwanamume mwenye umri wa miaka 50, mikono iliyofungwa kwa kamba na kuwekwa chini ya godoro.

Chakama sasa ni eneo rasmi la tukio la mauaji ya kinyama, likitajwa kuwa na uwezekano wa uhusiano na mtandao mpana wa ugaidi wa dini na vifo.

Kamishna wa Kaunti ya Kilifi Biwott, alisema serikali inaandaa mikakati ya kukabiliana na tishio la usalama lililojitokeza katika ardhi hiyo ya ekari 50,000 ya Chakama.

Ndani ya eneo hilo kubwa ndipo Mackenzie pia anasemekana alinunua kipande cha ardhi ambacho aligawia wafuasi wake.