Dkt Monda apoteza kazi kama Naibu Gavana wa Kisii
NA COLLINS OMULO
NAIBU Gavana wa Kisii Robert Monda amepoteza kazi yake baada ya maseneta kupiga kura ya kuunga mkono makosa manne aliyoshtakiwa na Bunge la Kaunti ya Kisii ambalo liliandaa ripoti ya kumng’atua.
Dkt Monda ambaye ni mbunge wa zamani wa Nyaribari Chache anakuwa Naibu Gavana wa kwanza kuondolewa afisini kupitia kura ya kutokuwa na imani naye tangu ugatuzi ulipoanza kufanya kazi mwaka 2013.
Alituhumiwa kwamba alipokea hongo ya Sh800,000 kutoka kwa Dennis Mokaya kwa ahadi ya kumtafutia kazi ya Meneja wa Mauzo katika kampuni ya maji ya Gusii (Gwasco).
Pia kosa jingine lilikuwa kumkamata na kumpeleka kortini ndugu yake, Bw Reuben Monda, kwa kukata miti katika shamba lao.
Maseneta walimkosoa sana kwa mienendo na vitendo vyake alipokuwa akijitetea.
Mnamo Jumatano ilikuwa zamu ya Bunge la Kaunti ya Kisii kujieleza mbele ya seneti nayo Alhamisi ikawa zamu ya Dkt Monda kujitetea.
Soma Pia: Monda roho mkononi Seneti ikianza kumjadili
Wakati kura zilianza kupigwa Alhamisi usiku ikikaribia saa sita usiku, maseneta kwa kishindo, walipiga kura ya kuunga mkono kwamba Dkt Monda alitekeleza makosa yote manne dhidi yake.
Kosa la kwanza lilikuwa ukiukaji wa Katiba ambapo maseneta 39 waliunga mkono huku watatu wakipinga naye mmoja akidinda kuchukua msimamo.
Maseneta idadi sawa na wa kwanza waliunga mkono kosa la pili lililohusu matumizi mabaya ya afisi yake. Walioupinga ni watatu huku mmoja akidinda, kama tu katika kosa la kwanza.
Kosa la tatu lilihusu ukiukaji wa maadili ambapo maseneta 35 waliunga mkono huku saba wakipinga naye mmoja akidinda kushiriki upigaji kura.
Nalo kosa la nne na la mwisho lilikuwa uhalifu chini ya sheria za kitaifa ambapo jumla ya maseneta 32 waliunga mkono huku 10 wakipinga naye mmoja akidinda kushiriki kura.
Aliyedinda kupiga kura alikuwa Seneta wa Kisii Richard Onyonka ambaye kutokea mwanzo alikuwa amesema hangeshiriki kura.
“Matokeo ya kura yanaonyesha kwa mujibu wa Kifungu 181 cha Katiba na Kipengele 33 cha Sheria ya Serikali za Kaunti, bunge la Seneti limeamua kumng’oa Dkt Robert Monda. Hivyo anaondoka afisini,” akasema Spika wa Seneti Amason Kingi.
Sasa Gavana Simba Arati ana siku 14 kumteua Naibu Gavana endapo Dkt Monda hataelekea mahakamani kupinga kutimuliwa kwake.
TAFSIRI NA: HASSAN WANZALA