Familia yaomboleza watatu waliofariki katika ajali baada ya kuhudhuria kesi ya ubakaji
FAMILIA moja kutoka kijiji cha Rukanga, Kaunti ya Kirinyaga inaendelea kuandamwa na simanzi baada ya watu watatu kufa kwenye ajali ya barabarani mnamo Julai 2.
Watatu hao walikufa katika ajali ya barabarani mjini Mutithi, eneobunge la Mwea. Waliopoteza maisha yao ni Jackson Mwangi, 20, mamake Susan Wanjiru, 45, pamoja na nyanya yao Beth Wanjiru, 75.
Walikuwa wametoka kortini Wangúru walipopatwa na ajali hiyo.
Kwa mujibu wa Msemaji wa familia John Gakotho, watatu hao walikuwa kwenye pikipiki wakirudi nyumbani baada kutajwa kwa kesi ya ubakaji dhidi ya Mwangi ambapo mamake na nyanyake walikuwa wameandama naye.
Mwangi ambaye alikuwa nje kwa dhamana alikuwa akiendesha pikipiki wakati wa ajali hiyo.
“Pikipiki yao iligongana na matatu na wanafamilia wote wakafa papo hapo. Sasa tunaomboleza na tumesalia na uchungu mwingi sana,” akasema Bw Gakotho.
Jamaa wa marehemu waliomba wahisani wawasaidie ili wawape wapendwa wao mazishi ya heshima.
“Hatuna pesa za kununua jeneza na kusafirisha miili kwa hivyo tunahitaji msaada wa dharura,” akaongeza.
Mkuu wa kanisa la Kianglikana Peter Gaitho naye alisema alikuja kufahamu mauti ya marehemu kwa masikitiko na akawaomba viongozi wa kieneo wasaidie kwenye maandalizi ya mazishi.
“Itakuwa gharama kubwa kuwapa marehemu mazishi ya heshima na viongozi wanastahili kuingilia kati na kusaidia. Nafahamu marehemu vizuri na vifo vyao vimenishtusha,” akasema Bw Gaitho.